Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI HASUNGA AIAGIZA COASCO KUKAGUA VYAMA VOTE VYA USHIRIKA


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Uongozi wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limetakiwa kukagua vyama vote vya Ushirika na kuwasilisha taarifa ya ukaguzi huo ofisi ya Waziri wa Kilimo kwa ajili ya hatua stahiki.


Mhe Japhet Hasunga (Mb), Waziri wa Kilimo ametoa agizo hilo jana tarehe 3 Juni 2019 wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa COASCO makao makuu sambamba na wakaguzi wa mikoa kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za COASCO makao makuu Jijini Dodoma.

Alisema kuwa lengo kuu la COASCO ni kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinakidhi matakwa ya kisheria na misingi ya kuanzishwa kwake ili wanaushirika na vyombo vyao vinakuwa salama kulingana na makubaliano, katiba na sheria zilizopo vile vile kusimamia sheria za ushirika na sheria za biashara wanazofanya ikiwa ni pamoja na sheria na sera za nchi na utawala bora.

“Nakuagiza Kaimu Mtendaji Mkuu kuhakikisha kuwa unakagua vyama vyote vya ushirika, mimi nisingependa nikikuomba ripoti ya ukaguzi uniambie eti kuna vyama vingine hujakagua na taarifa ya ukaguzi iwasilishwe katika ofisi yangu” Alisisitiza Mhe Hasunga

Aliongeza kuwa huduma za ukaguzi zinazotolewa na Shirika zinasaidia kuimarisha utawala bora katika vyama vya ushirika, kuwajengea imani wanachama wa vyama vya ushirika juu ya shughuli zinazofanywa na vyama vyao na hivyo kuongeza uzalishaji na kuboresha huduma zinazotolewa na vyama vya Ushirika.

Mhe Hasunga pia alimuagiza kaimu Mtendaji mkuu huyo kuhakikisha kuwa anapeleka mapendekezo ya viongozi waliopo katika vyeo vyao ili kuweza kuthibitishwa kwa wale wanaostahili.

Kwa kutambua mchango wa ushirika katika mageuzi ya kiuchumi hasa kwa wakati huu ambao serikali ya awamu ya tano inakusudia kuingia katika uchumi wa kati (kupitia agenda ya Tanzania ya Viwanda), Hivyo ili kufanikisha agenda hiyo wametakiwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato.

Aliongeza kuwa Vyama vya ushirika vina nafasi kubwa kuinua uchumi ikiwa tu usimamizi wa sheria na kanuni utaimarishwa kama inavyojidhihirisha katika serikali ya awamu ya tano.

Alibainisha pia kuwa, udhaifu katika usimamizi wa mifumo ya ufatiliaji ni moja ya changamoto zilizosababisha vyama vingi vya ushirika kutumbukia katika matatizo na kupelekea vyama vingi kufilisika.

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ni Shirika la Umma lililoanzishwa kwa Sheria Na. 15 ya mwaka 1982 kwa lengo la kutoa huduma za ukaguzi na Usimamizi kwa Vyama vya Ushirika Tanzania.

Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2005 ili kupanua wigo wa huduma za Shirika za Ukaguzi na Ushauri kutolewa kwa vyama vya ushirika pamoja na taasisi za Umma, makampuni binafsi, mabenki na wateja wengine.

MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com