WAZIRI wa mambo ya ndani nchini Kangi Lugola maarufu kama Ninja amefanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha polisi Gogoni kilichopo wilaya ya kipolisi Kimara ikiwa ni katika kuangalia utendaji kazi vituoni humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ukaguzi kituoni hapo Waziri Kangi amesema kuwa wamekagua na kuona ufanisi wa namna jeshi la polisi linavyotoa huduma kwa wananchi na kuwasikiliza maoni ya wananchi juu ya huduma wanazozipokea kutoka kwa jeshi la polisi.
Waziri Kangi amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kupitia ya ilani ya Chama cha mapinduzi iliyodhamiria kupambana na umaskini na changamoto ya ajira serikali ipo makini na wanahakikisha wananchi wanapambana na umaskini na tatizo la ajira.
Amesema kuwa vijana wengi wameamua kupambana na umaskini kwa kujiajiri kupitia pikipiki maarufu kama bodaboda lakini kumekuwa na malalamiko mengi ambayo yalifika hadi bungeni kwa vijana hao kuonewa, kupigwa na kunyang'anywa pikipiki zao.
Amesema kuwa kutokana na malalamiko hayo alitoa maagizo kwa vyombo husika juu ya bodaboda ambazo zinawezwa kukamatwa na kuwekwa katika vituo vya polisi; ambapo amesema kuwa bodaboda zinazostahili kukamatwa ni zile zilizohusika na uharifu, zilizohusika na ajali, zilizopotea na kuonekana na zile zilizookotwa na kueleza kuwa bodaboda nyingine zitakamatwa na makosa mengine ya usalama barabani kama vile kupakia abiria zaidi ya mmoja maarufu kama mshikaki na kutovaa kofia ngumu na mshtakiwa anaweza kutozwa faini ambayo italipwa ndani ya siku saba.
Kangi amesema kuwa baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha polisi Gogoni Wilaya ya Kimara na baada ya kuzikagua amejiridhisha kwa kukuta bodaboda zote zipo kwenye makundi aliyoyaainisha na amelipongeza jeshi la polisi.
Vilevile amesema kuwa kuna malalamiko ya vituo kukaa na watuhumiwa bila kupelekwa mahakama na kituo hicho kilikuwa kinaongoza kwa kukaa na mahabusu kwa muda mrefu na leo amekuta mahabusu 32, na amekutana na mahabusu 11 wanaohusika na kesi za mauaji na wamekaa magereza kwa miaka 7 na baadaye kurudishwa kituoni hapo ili kuweza kufutiwa kesi zao ila hadi sasa wapo kituoni hapo kwa miezi 6 jambo ambalo sio sahihi na ameongea na viongozi wa vituo hivyo na tatizo hilo litatatuliwa.
Kuhusiana na suala la mawasiliano hasa katika suala hilo la mahabusu kukaa vituoni muda mrefu amelichukua kama changamoto na watalifanyia kazi na kueleza kuwa kuhusiana na changamoto ya dhamana amempa maelekezo mkuu wa kituo cha polisi na kupinga kauli ya utakaa ndani hadi jumatatu ili hali kuna wadhamini.
Mwisho amesema kuwa kufuatia taarifa ya uwepo kwa ugaidi nchini, Waziri Kangi amehakikisha usalama wa wananchi na mali zao na kusema kuwa serikali ya Magufuli ipo macho na kwa wale wanaotumia mitandao ya kijamii kutisha wengine watapambana na sheria.