Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KIGWANGALLA AITAKA BODI YA UTALII TANZANIA KUTUMIA NJIA ZA KISASA ZA MAWASILIANO

WMU - Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt. Hamisi Kigwangalla ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iwekeze zaidi katika matumizi ya njia za kisasa za mawasiliano na mbinu rahisi zenye gharama nafuu kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.


Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Bodi hiyo iliyongezewa muda wa miaka 3 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Aprili 23 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuiongezea kipindi kingine cha miaka 3 na kuitaka bodi hiyo iendelee kubuni na kuongeza mbinu mpya za kutangaza utalii zitakazoleta tija na matokeo ya haraka.

Amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine za Wizara ili kuongezea idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania akiweka msisitizo katika matumizi ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano ili kupanua wigo wa kutangaza vivutio vya utalii kuliko ilivyo sasa.

“Bodi ya utalii mnapaswa kuona fursa zilizopo na kutimiza majukumu mliyopewa kwa tija na ufanisi zaidi, namna pekee ya kufikia malengo hayo ni lazima mtumie teknolojia na mbinu rahisi za mawasiliano  zenye gharama nafuu kutimiza majukumu yaleyale ya kutangaza vivutio vya utalii kisasa zaidi” Amesisitiza.

Ameipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri inayofanya ya kuendelea kuhamasisha shughuli za Utalii nchini na kuongeza kuwa kati ya vitu vilivyo iletea heshima sekta ya utalii Tanzania ni uwepo wa Kaulimbiu ya “TANZANIA UNFORGETTABLE” ambayo imekua chachu kwa taifa hasa katika kuitangaza sekta hiyo kitaifa na kimataifa.

Amesema kupitia kaulimbiu hiyo watalii wengi wanaoitembelea Tanzania wataendelea kukumbuka mambo mazuri na vivutio vizuri walivyoviona na kuendelea kuichagua Tanzania kuwa mahali pao pa kufanyia utalii.

Aidha, ametoa wito kwa Bodi hiyo kuendelea kuweka mazingira na kuongeza soko la bidhaa za utalii za Tanzania nje ya nchi kupitia maonesho ya kimataifa na kuwa na mkakati wa kulenga soko husika pamoja na kuonana na watu watakaouziwa bidhaa moja kwa lengo la kukamata soko katika maeneo kadhaa.

Pia ameitaka Bodi hiyo kuweka mkakati mahususi ya kukamata masoko mapya ya watalii kutoka nje ya nchi kutoka nchi za Marekani, Hispania, Urusi na nchi za Falme za Kiarabu zikiwemo za Dubai na Oman ambazo watu wake wakiwemo wasomi, wafanyabiashara, wanamichezo na watu maarufu wanapenda kwenda mapumziko ya muda mrefu na kutumia fedha nyingi kwa shughuli za utalii.

Katika hatua nyingine ameishauri Bodi hiyo kuwatumia watu maarufu na mashuhuri wakiwemo wasanii na wanamichezo watakaoalikwa mahususi kwa kazi maalum ya kutangaza utalii wa Tanzania.

“Licha ya changamoto ya ufinyu wa bajeti tunaweza kuweka mikakati ya kutangaza vivutio vyetu kwa tija na rahisi zaidi na kuifanya nchi yetu ijulikane na kuonekana na watu wengi , kuna mikakati tunaweza kuifanya mara moja tu ikadumu kwa muda mrefu, kama tukiwatumia watu mashuhuri wenye wafuasi wengi wakatembelea vivutio vyetu tuna uhakika watu wengi zaidi watafuatilia ziara zao na kufuata walichokichagua, lazima tuweke mikakati ya kuwaleta watu mashuhuri walau 5 kwa mwaka ambao sisi tutawaalika, tutapata mafanikio makubwa sana ndani ya muda mfupi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constatine Kanyasu akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo amemshukuru Rais kwa kuiongezea kipindi kingine cha miaka cha miaka 3.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 3 imefanya kazi kubwa licha ya changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo akisisitiza kwamba uwepo wa changamoto hizo ni uhalali wa kuwepo kwa bodi hiyo.

Amesema kuzinduliwa rasmi kwa bodi hiyo kutaifanya itekeleze majukumu yake kwa kasi kubwa zaidi akisisitiza kwamba kupitia bodi hiyo sekta ya Utalii Tanzania  itasonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.

Mhe. Kanyasu ameitaka bodi hiyo iongeze juhudu ya kutangaza utalii na kupanua wigo wa kutangaza soko la utalii ndani na nje ya nchi akisitiza akisisitiza kwamba bado kuna mazao mengi ya utalii ambayo hayajavunwa na endapo bodi itafanya kazi yake ipasavyo Tanzania itapata mafanikio makubwa kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Mwenyekiti  wa Bodi ya Utalii Tanzania Jaji (Mst) Thomas Mihayo akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa Bodi hiyo amemshukuru Rais hiyo nafasi nyingine akiahidi kwamba  bodi yake itafanya kazi kwa kasi na bidii zaidi ili kutimiza malengo ya kuitangaza Sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.

Jaji Mihayo amesema kuwa Bodi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa Wizara na kuitangaza kikamilifu sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.

Bodi hiyo yenye wajumbe 6 iliongezewa muda wa kuhudumu wa miaka 3 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  Aprili 23, 2019.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com