Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi Baraza la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu huku akilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano ili kuleta tija na mafanikio makubwa kwa Watu wenye Ulemavu nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo alisema kuwa baraza linajukumu kubwa katika kuhakikisha usimamizi wa sekta ya watu wenye ulemavu pamoja na kuishauri Serikali juu ya masuala mbalimbali ya kundi hilo maalumu.
“Mtambue nafasi mliyopewa ni dhamana kubwa katika kuwahudumia watu wenye ulemavu ambao ni takribani asilimia 5 ya watanzania, hivyo ni vyema mkashirikiana na Serikali kubuni mikakati itakayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili wenye ulemavu”, alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010 na Sheria hiyo imeeleza majukumu ya Baraza ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri.
“Ni matumaini yangu mtakuwa washauri wazuri wa masuala ya watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa kwa wote na si maslahi binafsi,” alisisitiza Mhagama.
Sambamba na hilo alimpongeza Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Dkt. Lukas Kija kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Wajumbe wengine kutokana na uaminifu na uwezo walionao katika kusimamia masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanapata haki zao za msingi na kwa ajili ya ustawi wao katika Nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, uchumi, kuwa na miundombinu rafiki pamoja na nyenzo za kujimudu.
Aidha Waziri Mhagama alitoa rai kwa watendaji wa Baraza hilo kuwa na miongozo yote inayohusu masuala ya Watu wenye Ulemavu itakayo wawezesha kufanikisha utendaji wao wa kazi.
Kwa Upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa Serikali katika mwaka 2019/2020 itaanza mapitio ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la ushauri kwa Watu wenye Ulemavu Dkt. Lukas Kija alieleza kuwa wapo tayari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia haki na ustawi wa Watu wenye Ulemavu.
Aliongeza kuwa Baraza hilo lipo tayari kutoa ushauri na hoja zenye tija kwa Serikali juu ya masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu.
Pia, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Andrew Massawe alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Baraza hilo na kufanya kazi pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu nchini ikiwemo migogoro na migongano kwa wadau.
Uzinduzi wa Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu umefanyika Juni 2, 2019 jijini Dodoma ambapo Baraza hilo litaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu (2019 hadi 2021) likiongozwa na Mwenyekiti Dkt. Lukas Kija. Awali Baraza hilo lilikuwa likiongozwa na Dkt. Edward Bagandanshwa ambalo limemaliza muda wake mwaka 2017.
MWISHO