WAZIRI MKU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji na biashara.
Amesema mpaka sasa, hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 27, 2019) jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la uwekezaji la mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
”Miongoni mwa hatua hizo ni uwepo wa usafiri wa uhakika na wa haraka wa abiria na mizigo kwa kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (Standard GaugeRailway).”
Pia, Waziri Mkuu amesema uwanja wa ndege wa Dodoma umeboreshwa na kuruhusu ndege kubwa na ndogo kutua usiku na mchana.
”Mashirika ya ndege yanayotoa huduma yameongezeka na maandalizi ya awali ya ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege katika eneo la Msalato yanaendelea.”
Waziri Mkuu amesema mkoa wa Dodoma una barabara za kuaminika za kiwango cha lami zinazoiunganisha na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha huduma za afya na Dodoma kuna hospitali ya Benjamin Mkapa yenye uwezo kama wa Muhimbili na Mloganzila.
Amesema ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji ‘Stiegler’s Gorge’wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115, utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.
“Mradi huo utaongeza upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda na uwekezaji nchini ikiwemo na katika mkoa wa Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (The Blue Print) utakaoanza Julai mosi mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema anatarajia kuwa kongamano hilo litawezesha kupatikana kwa wawekezaji mahiri kwa maendeleo ya uchumi na wananchi wa Tanzania.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge alisema katika azma ya Selikali ya kujenga uchumi wa viwanda wameandaa kongamano hilo ili kutangaza fursa zilizopo.
Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Dodoma Fursa Mpya Kiuchumi Tanzania, Wekeza Dodoma Tukufanikishe’, inatanabaisha nafasi ya mkoa huo kwa sasa na baadaye.
Dkt. Mahenge alitaja baadhi ya fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Dodoma kuwa ni pamoja na uwepo wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, viwanda na taasisi (afya, elimu).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin