WAZIRI MKUU AUSHUKURU UONGOZI WA KANISA KUTOA ENEO KWA AJILI YA UJENZI WA SHULE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameushukuru uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi kwa kutoa sehemu ya eneo lake na baadhi ya majengo kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Jimbo Katoliki la Lindi limetoa eneo hilo lilipo katika Parokia ya Mnacho wilayani Ruangwa ambalo awali ilikuwa shule ya msingi ya Mnacho sasa imebadilishwa na kuwa sekondari.

Waziri Mkuu ametoa shukurani hizo leo (Jumapili, Juni 2, 2019) alipokwenda kwenye kanisa Katoliki la Theresia wa Mtoto Yesu, Parokia ya Mnacho kuwasalimia waumini.

Amesema lengo la kuibadilisha shule hiyo kuwa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ni kuwawezesha watoto wa kike wa Wilaya hiyo kusoma katika mazingira mazuri.

Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Mkewe Mary amesema shule hiyo ya bweni itawapunguzia vishawishi watoto wa kike, hivyo kuwawezesha kutimiza malengo yao.

Awali, uongozi wa Parokia hiyo uliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu pamoja na miundombinu katika wilaya hiyo.

Naye, Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amewaomba viongozi wa dini washikamane na wahakikishe wanatatua changamoto ya mmomonyoko wa maadili.

Amesema changamoto ya mmomonyoko wa maadiji katika jamii hususani kwa vijana ni kubwa, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba wanawarejesha kwenye maadili bora.

Kadhalika, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia na amesema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.

Shughuli zinazoendelea katika shule hiyo ni pamoja na ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa, maabara na nyumba nne za walimu ambazo tayari ujenzi wake umekamilika.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post