Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA UJENZI YASHAURIWA KUONGEZA KILO ZA MIZIGO KWENYE BOTI


Spika wa Bunge, Job Ndugai ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kuangalia  namna ya kuongeza kilo zinazopimwa kwa abiria wanaotaka kusafiri na boti kwenda Zanzibar kutoka  kilo 20 za sasa.

Ndugai amedai kwamba kilo hizo ni ndogo hivyo iko haja ya kuliangalia upya suala hilo la mizigo kwani kilo 20 hata begi la mwanafunzi tu linafikisha , hivyo basi  liangaliwe upya ili kuondoa adha kwa wasafiri.


Kauli hiyo ya Spika imekuja baada ya kujibiwa swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maryam Salum Msabaha, kudai kuwa kuna changamoto bandarini na kwamba hata kilo 10 zinatozwa fedha hali inayosababisha malalamiko kwa wananchi.

Mbunge huyo alihoji ni vigezo gani ambavyo vinatumika kwa mizigo ya biashara na mizigo binafsi kwa wasafiri.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alisema vigezo vipo mwongozo wa tozo TPA na kwamba tatizo linaonekana ni uelewa.

"Niwaelekeze Bandari watoe elimu ya kutosha kwa wananchi wanaotumia usafiri kwenda Zanzibar ikiwamo hili la uzito wa kilo 21 na kuendelea ndio unatakiwa kutozwa, sio nia ya serikali kuona wananchi wake wanalalamika," alisema.

Kufuatia majibu hayo, Spika Ndugai, alisema kama kweli kilo 21 ndio kiwango cha chini ipo haja kuangalia kwenye boti.

"Maana kilo 20 hata sanduku la mwanafunzi linazidi, hata baadhi ya mashirika ya ndege yanatoa zaidi ya kilo 20, sasa kwenye boti kilo 20 ni kidogo sana."

Aliongeza "Ipo haja ya kuangalia kama sio sheria ni kanuni tu...Mtu akibeba mihogo mitatu kilo 20 tu anakuwa ameshavuka kwa hiyo tuliangalie, hawa wenzetu wanaotoka Zanzibar wapate raha kidogo na imekuwa kero kwa wananchi serikali iliangalie hili."

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alisema abiria wanaokwenda Zanzibar kwa boti hulipishwa ushuru wa Bandari kwa mizigo hata kama boksi la kilo 10 au kilo 20 za mchele kwa Sh. 9,750.

"Je, ni mizigo gani ambayo abiria anapaswa kulipia ushuru huo wa Bandari (Wharfage)," alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kwandikwa alisema TPA huikusanyi tozo yoyote kwa abiria ambao wana vifurushi binafsi vyenye uzito au ujazo mdogo wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti eneo la 'Baggage room.

Aidha, alisema abiria wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti ambao hutozwa ushuru katika eneo la 'Bagage room' ni wale tu wanaokuwa na mizigo mikubwa tena kwa madhumuni ya kibiashara.

Alitoa wito kwa wateja wote wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti wahakikishe kuwa mizigo yao inapimwa kabla ya kupakiwa ili wajue uzito wake unaostahiki kutozwa ushuru.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com