Meneja wa Tigo Tanzania, Kanda ya Pwani kusini, Pwani Kaskazini na Kinondoni, Deogratius Daud, akiongea na wakazi wa Chalinze (hawapo pichani ) wakati wa hafla ya uzinduzi huo.
Meneja mauzo wa Tigo Tanzania, mkoa wa Pwani Kanda ya Pwani Kaskazini na Pwani ya Kusini Alpha Peter, akiongea juu ya huduma ya inteneti ya 4G kwa wakazi wa Chalinze.
Baadhi ya wakazi wa Chalinze wakisajili line zao kwa mfumo wa alama za vidole wakati wa hafla hiyo ambapo pia wengine walibadilisha laini zao kuingia kwenye mtandao wa 4G.
Baadhi ya wakazi wa Chalinze wakipata maelezo kutoka kwa Maofisa wa Tigo kuhusu huduma mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa na kampuni ikiwemo matumizi ya mtandao wa 4G
---
Wakazi wa mji wa Chalinze mkoani Pwani sasa wataweza kupata huduma bora zaidi za kupiga simu, Intaneti na huduma za kifedha kupitia simu kutoka Tigo kufuatia uzinduzi wa mtandao wa 4G wilayani humo.
Akizindua mnara wa 4G kwenye kata ya Bwilingu, Meneja wa Tigo, Deogratius Daudi amesema uboreshaji wa mtandao kutoka 3G kwenda 4G unatarajiwa kufungua fursa mpya za kibiashara ambazo zitakuza maendeleo ya kiuchumi na kuinua maisha ya watu katika eneo hilo.
“Kwa kuzingatia kwamba Chalinze ina shughuli nyingi muhimu za kiuchumi na ni kiunganishi muhimu na maeneo mengine ya nchi, sasa ni wakati wa wakazi wa Chalinze kutumia Intaneti yenye spidi kikamilifu ili kuendeleza biashara zao,” alisema Daudi.
Mtandao wa 4G wa Chalinze ni wa saba kati ya 52 ambayo imepangwa kuboreshwa kuwa ya 4G hususani katika Kanda ya Ziwa, Pwani, Kusini na Kaskazini.
Uzinduzi huo unaenda sambamba na ofa maalum kwa ajili ya wateja watakaobadili laini zao kwenda mtandao wa 4G watazawadiwa vifurushi vya 4GB vya Intaneti ya bure itakayotumika ndani ya siku 30. Vilevile, wateja watakaonunua kifurushi chochote cha intaneti kwenye mitandao iliyoboreshwa kutoka 2G kwenda 3G watazawadiwa MB100 kila wanaponunua kifurushi. Ofa zote mbili zitadumu kwa siku 30 baada ya uzinduzi wa mnara husika.
Daudi alisema kufuatia uzinduzi wa mtandao wa 4G wilayani Chalinze, wateja sasa wataweza kunufaika na huduma mbalimbali za kiubunifu kutoka Tigo kama vile “Saizi Yako” ambayo inawapatia wateja ofa mbalimbali za SMS, Intaneti na kupiga simu kulingana na mahitaji na matumizi ya mteja. Kwa mfano mteja anayetumia dakika nyingi zaidi kuliko Intaneti na SMS atapata kifurushi cha dakika za muda wa maongezi. Mteja anayetumia zaidi Intaneti kuliko dakika za maongezi na SMS atapata kifurushi cha Intaneti kinachoendana na matumizi yake.
Tigo inaendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa hususani 4G+ ili kukidhi mahitaji makubwa ya data na Intaneti yenye kasi kutokana na ongezeko la matumizi ya simu janja za bei nafuu.
“Uboreshaji wa mtandao huu kutoka 3G kwenda 4G unatarajiwa kuboresha maisha ya wananchi kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia mtandao wa Intaneti hususani huduma za kibiashara, kiafya, kielimu na huduma za kulipia tozo mbalimbali za serikali,” alisema Daudi.
Minara mingine itakayoboreshwa Kanda ya Pwani na inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni ni pamoja na Bagamoyo, Tanga, Morogoro na Mtwara.