Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMDT YAWAJENGEA UWEZO WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI


Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Biashara Oliver Vengula akizungumza na wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maafisa biashara wa mikoa ya Singida na Manyara juu ya mwongozo mpya wa uendeshaji wa Mabaraza ya biashara, wakati wa warsha ya
siku moja ya kuwajengea uwezo watendaji hao iliyokuwa imeandaliwa na taasisi ya kuendeleza mifumo ya masoko ya kilimo nchini – AMDT. 
Mkuu wa Wilaya ya Babati Bi. Elizabeth Kitundu akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuendesha Mabaraza ya Biashara watendaji wa sekta ya umma kutoka mikoa ya Manyara na Singida. 
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula akitoa uzoefu wa utendaji wa mabaraza ya biashara katika wilaya yake wakati wa warsha hiyo. 
Mwezeshaji wa Warsha hiyo Dr Donath Ollomi akifafanua mbinu mbalimbali za uendeshaji mabaraza ya biashara na namna mabaraza yanavyoweza kutumika kama majukwaa ya majadiliano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. 
Bi Tertula Swai – Mtaalamu wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara wa AMDT, akifafanua jambo wakati wa warsha hiyo. 
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bwana Joseph Mkirikiti akisisitiza jambo kwa watendaji wenzake wakati wa warsha hiyo, ambapo
alisisitiza kwa viongozi wenzake kuisaidia serikali ya awamu ya tano kuweza kutekeleza ahadi zake na hasa kwa kuweka mazingira bora na Rafiki ya kibiashara katika maeneo yao
Baadhi ya Washiriki wa mkutano h uo wakichangia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakijadiliwa.
Washiriki wakiwa katika picha ya Pamoja mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo.

Na Dixon Busagaga wa Michuzi TV Manyara. 
Proramu ya kuendeleza mifumo ya Masoko katika Kilimo (AMDT) imeanza kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa ngazi za  Wilaya na Mikoa ili kuongeza chachu ya kufanya mijadala baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,lengo likiwa ni uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji Biashara katika maeneo yao.

Hatua hii inakuja ikiwa takribani mwezi mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt  John Pombe Magufuli azitake serikali za mitaa kutilia mkazo mabaraza ya Biashara kwenye maeneo yao.

Katika mkutano uliofanyika wilaya ya Babati mkaoni Manyara na kuwakutanisha Wakuu wa wilaya ,Wakurugenzi wa Halmashauri,Wenyeviti wa Mabaraza ya Biashara kutoka wilaya za Mikoa ya Singida na Manyara ,Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akaziasa Vyombo vinavyotunga sheria kuwashirikisha wadau kutoka sekta Binafsi.

Akisoma hotuba ya ufunguzi  kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa ,Mkuu wa Wilaya ya Babati Bi Elizabeth Kitundu ,Mnyeti alisema ipo haja kwa mamlaka zinazosimamia utungaji wa Sheria katika ngazi za wilaya, miji na majiji kuhakikisha zinawashirikisha wadau  muhimu, hususani kupitia mabaraza ya biashara.

“ Tunayochangamoto kubwa sana ya fursa ya ajira, kati ya wahitimu zaidi ya laki nane wanaohitimu kila mwaka ni asilimia kumi tu ndio hupata ajira, hivyo tunalojukumu kuhakikisha kupitia mabaraza ya biashara tunatengeneza fursa nyingi ili kundi hili liweze kujiajiri ” alisema Mnyeti. 


Mnyeti ameongeza kuwa licha ya hali ya uchumi nchini kuimalika,bado kumekuwepo na tofauti kubwa sana ya kipato kati ya kundi la masikini na  wale waliojaliwa kupata kipato . 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Hanang Joseph Mkirikiti alisema ili ndoto na matamanio ya serikali ya awamu ya tano iweze kutimia ni lazima watendaji wa serikali na hususani katika ngazi za wilaya kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha wanamsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli. 

“ Inasikitisha sana wengi wetu hatufanyi vile Mh. Rais anavyotaka tufanye na badala yake tumekuwa watu wa matamko tu na kuweka mbele vyeo vyetu hali ambayo imezorotesha mahusiano yetu na sekta binafsi” Alisema Mkirikiti. 

Mkirikiti ameongeza kuwa ni jambo la ajabu na kusikitisha pale matatizo ambayo yangeweza kutatuliwa katika ngazi ya wilaya yanamfikia kiongozi Mkuu wa nchi kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi. 

“Hii siyo sawa…tunaowajibu kuhakikisha mazingira mazuri ya biashara yanakuwepo katika maeneo yetu,…nitoe rai kwa wakuu wenzangu wa wilaya tukitoka hapa tubadilike na tumsaidie mheshimiwa Rais katika kuhakikisha anawapatia watanzania maendeleo. Aliongeza Mkirikiti. 

Naye Naibu Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Bi. Oliver Vengula alisema kwa sasa baraza hilo limetoa mwongozo mpya ambao ndio utakaokuwa ukitumika katika kuendesha mabaraza. 

“Majuzi tumemuona mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwaita wafanyabiashara kutoka wilaya zote hapa nchini kwa ajili ya kujadiliana nao namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara, na kama mtakuwa mmegundua sehemu kubwa ya mambo yaliyojadiliwa au kulalamikiwa mengi yanatuhusu sisi watendaji wa huku chini, hatukutekeleza wajibu wetu…..,tubadilike sasa na tuanze kuyatumia mabaraza ya biashara kumaliza kero mbalimbali",alisema Bi.Vengula 

Waandaaji wa mkutano huo ambao ni Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Kilimo nchini (AMDT) kupitia Mwenyekiti wake wa Kamati ya Ufundi Mike Laizer walisema malengo ya warsha hiyo yalikuwa kuwajengea uwezo watendaji hao wa sekta ya umma pamoja kutambua vikwazo vinavyoikabili sekta ya umma katika kutekeleza majukumu yake. 

“AMDT  imelenga kuboresha mifumo mbalimbali ya kimasoko ili iweze kumsaidia mkulima na hususani mkulima wa mazao ya alizeti, mahindi na mikunde,Tumelenga kuwa na mazingira wezeshi kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa kuwa na mazingira rafiki ya kibiashara baina ya pande husika," alisema Laizer 

Akizungumza kuhusiana na mpango huo, Mtaalamu wa kuendeleza Mifumo ya Masoko wa AMDT, Bi Tertula Swai amesema mpango wa kuwakutanisha watendaji hao wakuu kutoka katika wilaya tofauti hapa nchini umelenga kuwajengea uwezo na kuweka mifumo endelevu ya mabaraza ya biashara katika kutatua kero mbalimbali. 

"Tunataka kuona kupitia mifumo tunayoiweka sasa mabaraza haya ya biashara yanakuwa endelevu na utendaji wake unakuwa wenye ufanisi hata baada ya kuisha kwa mradi wa AMDT.” alisema Bi Swai.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com