Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Naibu Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso amesema Wizara yake itashirikiana na TAKUKURU ili kujiridhisha katika utekelezaji mradi wa Maji kijiji cha Masange Wilayani Kondoa mkoani Dodoma Uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 433 baada ya kupewa majibu yasiyojitosheleza na Mkandarasi wa Mradi huo.
Naibu Waziri Aweso ameyasema hayo Julai 18,2019 katika kijiji cha Masange Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo alipofanya ziara ya kukagua na kujionea mradi wa Maji kijiji cha Masange uliogharimu kiasi cha Sh.Milioni mia nne thelathini na tatu,laki mbili,themanini na nane elfu,mia tano ,arobaini nane[433,288,548].
“Haiwezekani tukauziwa mbuzi kwenye gunia,lazima kukagua na kujionea,baada ya kupewa majibu ya kusuasua hivyo TAKUKURU tutashirikiana nao kubaini ubadhilifu,na mkandarasi asilipwe mpaka tufanye uchunguzi tujiridhishe”alisema Aweso.
Hali hiyo imekuja baada ya Mkandarasi wa mradi huo wa Maji kampuni ya Best One kwa kushirikiana na wataalam wa sekta ya Maji wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kutoa majibu yasiyoridhisha kuhusu matumizi ya fedha zilizotumika katika mradi huo .
Mhe.Aweso amepiga simu mbele ya wananchi kuulizia taratibu za upatikanaji wa Gari la kuchimba visima .
Mbunge wa Kondoa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dokta.Ashatu Kijaji amesema yupo tayari kufanya kazi hata saa sita usiku na walichomwagiza wananchi wake ni kutatua kero ya Maji .
Wananchi wa Mtaa wa Masange wamesema adha kubwa inayowakabili ni maji hivyo ni vyema serikali ikafanya mchakato haraka kutatua kero hiyo.
Awali ,akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Masange mbele ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso,Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji vijijini[RUWASA]Wilaya ya Kondoa Mhandisi Falaura Seleman Kikusa amesema mradi wa Maji Masange ulianza tangu tarehe 15,Disemba,2014 na kuzinduliwa rasmi tarehe 13,Septemba ,2016 kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru huku ukigharimu zaidi ya Tsh.Milioni 433 .
Aidha amebainisha kuwa muda wa utekelezaji wa Mradi huo kwa mujibu wa Mkataba ni kipindi cha miezi mine kuanzia tarehe 15,Disemba,2014,hadi 15,Machi,2015 hivyo kutokana na changamoto mbalimbali hususan kuchelewa kwa malipo ya madai ya mkandarasi,mradi uliongezewa muda wa utekelezaji na kukamilika rasmi mnamo tarehe 7,Juni,2018.
Mhandisi Kikusa ameendelea kufafanua kuwa upatikanaji wa Maji katika kijiji cha Masange haukidhi mahitaji halisi ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho kwani huduma ya maji imekuwa ikipatikana kwa mgao kwa vitongoji kwa masaa manne hadi matano.
Amesema chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo unatokana na changamoto kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa wakazi pamoja na kukua kwa mji wa Masange ,Uwezo wa chanzo cha Maji [lita 119,577.6 kwa siku]kuwa mdogo ikilinganisha na mahitaji halisi ya Maji ya sasa [zaidi ya lita 141,560 kwa siku] na changamoto nyingine ni usimamizi usio mzuri kutoka kwa timu ya mhandisi .
Hata hivyo mkandarasi wa mradi hadi kufikia sasa alishalipwa kiasi cha sh.347,421,000 kati ya gharama 433,288,548 na zilizobaki kwa mujibu ya makubaliano ya mkataba ni Tsh.120,609,648.