Na Sultani Kipingo wa Michuzi TV.
Mfanyabiashara maarufu nchini Azim Dewji na Waandishi Watatu wa vituo vya televisheni ya ITV,Chanel Ten na Azam TV wamepata ajali leo Julai 27,2019 majira ya asubuhi baada ya gari lao kuacha njia na kuingia vichakani kijiji cha Nyamwinywili,Rufiji mkoani Pwani.Akiongea na Michuzi TV, Dewji, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shia Ithnaasheri, amesema anaendelea vyema na matibabu hospitalini hapo, huku akitoa shukurani kwa madaktari katika Hospitali ya Misheni ya Mchuki alikopatiwa matibabu ya awali, pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya afya Dkt. John Kiang’u Jingu na Wasaidizi wake ambao amesema walikatisha safari ya kuelekea Rufiji ili kumfikisha hospitali hapo.
Dewji, ambaye aliwahi kuwa mfadhili wa simba miaka ya 1990, amewashukuru pia madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa cha MOI kwa kile alichoeleza ni weledi wa hali ya juu kwa huduma bora alizopatiwa toka alipopelekwa hapo na anazoendelea kupatiwa.
“kwa kweli huduma za hapa Muhimbili hazina tofauti na huduma utazopata katika hospitali yoyote kubwa duniani”, amesema Dewji. “Kwa kweli nimeshangaa na nawashangaa wale ambao baada ya kupata matatizo hawaji hapa Muhimbili. Pako vizuri kwa kweli…”
Akielezea chanzo cha ajali, anasema tairi lilipasula na kusababisha dereva wake kuacha barabara na kuingia porini kabla ya kugonga mfereji na kusababisha gari kupaa juu na liliporudi ndipo yeye akaumia uti wa mgongo.
“Wengine wote walitoka salama. Kwa kweli ajali ni majaaliwa ya Allah. Tulikuwa tumebakiza dakika kama ishirini hivi kufika kwenye hafla ya kuweka jiwe la Msingi la Rufiji Hydro Power Project ndipo tukapatwa na kadhia hiyo”, amesema Dewji.
Amesema alikuwa ndani ya gari akiwa na wanahabari kadhaa ambao aliwapa lifti baada ya kuachwa na gari maalumu waliloandaliwa, na kuongeza kwamba anashuru wanahabari hao wote wako salama na waliendelea na safari kwenda kwenye eneo la sherehe.
“Nilienda kumsapoti Mheshimiwa Rais wetu na tutaendelea kumsapoti” alisema Azim na kuongezea: Tunamwombea kila siku Mungu amlinde na maadui wake ili aendelee kutuongoza kufikia Tanzania ya asali na maziwa ambayo imeshaanza kuonekana…”
Madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Misheni ya Mchuki wakimpatia Azim Dewji huduma alipofikishwa hapo baada ya kupata ajali
Madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Misheni ya Mchuki wakiendelea kumpatia Azim Dewji huduma na uangalizi alipofikishwa hapo baada ya kupata ajali
Azim Dewji akisubiri kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupata rufaa katika hospitali ya Micheni ya Mchuki alikopatiwa huduma na uangalizi wa awali
Social Plugin