Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI SEIF ALI IDDI AITAKA TANTRADE KUIMARISHA MITANDAO YA KUWASAIDIA WAFANYABIASHARA

Na Mwandishi Wetu,MAELEZO

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuendelea kuimaisha mitandao na mifumo ya biashara nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kuwa na uhakika wa masoko bora ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.

Akifunga Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) leo Alhamisi (Julai 11, 2019) Balozi Idd alisema Maonesho hayo ya mwaka huu yameonesha dhamira na mwelekeo wa Serikali katika kutumia fursa biashara na viwanda katika kujenga uchumi imara pamoja na kutengeneza ajira kwa wananchi.

Balozi Idd alisema ni wajibu wa TANTRADE kutumia fursa za uwepo wa makampuni ya wazalishaji, wauzaji na wafanyabiashara kutoka nje wanaoshiriki katika maonesho hayo kuweza kujenga mitandao imara ya mahusiano na ushirikiano kwa wafanyabiashara wa ndani ili kuweza kuwatafutia masoko ya bidhaa zao ambazo kwa sasa zimeanza kuzalishwa katika viwango bora nchini.

“Nawapongeza TANTRADE kwa juhudi zenu za kuanzia klinilki za biashara, na hili limewezesha wafanyabiashara wetu kuweza kukutana na wanunuzi mbalimbali ambao huweza kuwapa uzoefu wa namna bora zaidi ya kuzalisha bidhaa zenye kukithi viwango na ubora unaotakiwa” alisema Balozi Idd.

Aidha Balozi Idd alisema Serikali kwa sasa inatekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mfumo Udhibiti wa Biashara Nchini (Blue Print), ambao umekusudia kuondoa changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hivyo aliitaka TANTRADE kushirikiana na wadau na wazalishaji wa sekta binafsi ili kuiwezesha sekta ya biashara kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Balozi Iddi pia aliitaka TANTRADE kuweka utaratibu wa kufuatilia oda za maombi mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ili kuendelea kupanua wigo wa soko la bidhaa za Tanzania nje ya nchi ambalo kwa sasa limeendelea kupanuka kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali.

Balozi alisema ni wajibu wa Watanzania kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani ili kuziwesha kupata masoko ya uhakika kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutatoa fursa ya kuweza kutambulika kwa haraka pamoja na kumudu changamoto ya ushindani wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.

Alisema kuwa maonesho hayo ya 43 yamethibitisha uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania katika kutengeneza na  kuzalisha bidhaa mbalimbali kwani idadi ya washirki wa maonesho kutoka nje ya nchi imeweza kuongezeka kutoka makampuni kutoka nje 2956 mwaka 2018 hadi kufikia 3250 mwaka 2019, hivyo kudhibitisha uwezo wa serikali katika kusimamia sekta ya biashara nchini.

Balozi Idd anasema kuwa Makampuni ya wafanyabiashara ya Tanzania yaliyoshiriki maonesho hayo yanapaswa kupata uzoefu na uelewa mkubwa katika namna bora zaidi ya kusimamia na kuratibu sekta ya biashara nchini katika viwango bora ili kuweza kutengeneza masoko ya uhakika katika nchi za nje.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuanza kufanya mapitio ya sera na sheria mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikileta changamoto mbalimbali kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda na biashara inaleta tija katika ukuaji uchumi nchini, Serikali imekusudia kuweka msisitizo katika kujenga uchumi jumuishi kwa kuziweka sekta ya uvuvi, kilimo na mifugo kuwa kipaumbele muhimu katika kuzitumia rasilimali mbalimbali zilizopo katika sekta hizo katika kutengeneza ajira kwa wananchi walio wengi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com