Na Gasto Kwirini wa Polisi Arusha
Katika operesheni ya ukaguzi wa magari ambayo bado inaendelea leo tarehe 10.07.2019 muda wa saa 06:00hrs asubuhi Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP)Joseph Bukombe akiwaongoza Askari katika barabara ya Arusha – Kiteto walifanikiwa kukamata Basi lenye Namba za Usajili T. 735 AEM mali ya Kampuni ya COAST LINE likiwa limepakia abiria 95.
Basi hilo ambalo linafanya safari zake kati ya Arusha na Kiteto lilikua limepakia abiria 67 ambao walikua wamekaa kwenye siti, 25 walikua wamesimama, kati yao Abiria wa kawaida walikua 10 na Wanajeshi 15. Pamoja na hao walikuepo Dereva, kondakta, fundi na Msindikizaji wa basi hilo ambapo wanafanya idadi yao kuwa 95.
Akizungumza na Abiria wa Basi hilo Mkuu huyo wa Usalama Barabarani amewataka kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wanapoona Basi limezidisha abiria, mwendo mkali na kutokubali kupanda basi ambalo limejaa.
Aidha ametoa wito kwa wamiliki wa Mabasi kuwasimamia Wafanyakazi wao hasa madereva na Makondakta ili waweze kufuata sheria bila kushurutishwa.
“Wamiliki tokeni majumbani, fanyeni ukaguzi wa kushtukiza kuliko kulaumu kila mara tunawakamata kwa kuwaonea, mmiliki atakapowasimamia watu wake Jeshi la Polisi halitaangaika na mtu kumkamata” Alisisisitza RTO Bukombe.
Meneja wa Mabasi ya Coast Line Bwana Petro Amsi Stanley amepongeza Operesheni hiyo inayoendelea kufanywa kwani itasaidia kuwadhibiti Madereva na Makondakta wanaofanya kazi bila kufuata sheria kwa sababu Wamiliki na Mawakala wanakua hawana taarifa za abiria kuzidi kwenye mabasi yao.
Pia amempongeza Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa ufasaha.
“RTO huyu anajiamini na anafanya kazi yake kwa ufasaha mkubwa, na hii imebabishwa na kutokua na ushirika na Mtu hasa wamiliki wa Vyombo vya moto, hivyo tunampongeza kwa Opereshini hii anayoendelea kuifanya”. Alisema bwana Esto.
Basi hilo limefikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kufanyiwa Ukaguzi zaidi.
Aidha Mkuu wa wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha ameamuru wakala wa basi hilo awatafutie abiria wote waliozidi usafiri mwingine.
Sambamba na hilo, Dereva na Kondakta wa basi hilo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano, mara baada ya Upelelezi kukamilika watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Social Plugin