Kwa mara ya kwanza Barani Afrika na kwa mara ya kwanza katika utendaji wake Benki ya Dunia, kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, wamefanya zoezi la mezani la Kupima uwezo utekelezaji wa Mpango wa Kujiandaa na kukabili Maafa kwa kutumia maafa ambayo yamepata kutokea kweli hapa nchini, ambapo zoezi hilo limetumia maafa ya mafuriko mkoani Morogoro, wilayani Kilosa kwa mwaka 2014 na mwaka 2016. Mazoezi mengine ya mezani ya kujiandaa na kukabli maafa hutumia matukio ya maafa ya kinadharia na hufanyika kabla ya maafa kutokea.
Mtaalam Mwandamizi wa menejimenti ya Maafa, kutoka Benki ya Dunia, Elad Shenfeld, amebainisha mambo matano ambayo yameifanya Benki hiyo kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufanya zoezi hilo, kuwa ni Uwajibikaji na uwazi katika kuratibu shughuli za menejimenti ya maafa unaofanywa na serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, uwepo wa Sheria ya Maafa, ambayo ni Sheria ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2015, Mpango wa Taifa wa kujiandaa na Kukabili maafa wa mwaka 2012, Uwezo, Weledi na Uwajibikaji wa watumishi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa katika menejimenti ya maafa pamoja na Ushirikiano mzuri wa serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia Tanzania na Kanda ya Afrika katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.
Akiongea mara baada ya kufunga zoezi hilo mjini Arusha, tarehe 16, Julai, 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amebainisha kuwa nchi nyingi barani Afrika ikiwemo Tanzania zimekuwa zikifanya mazoezi ya kujiandaa na kukabili maafa kwa kutumia nadharia za maafa yanoyoweza kutokea, lakini zoezi hilo ni tofauti kwani limejikita kwa maafa ambayo yamewahi kutokea kweli hapa nchini.
“Zoezi hili ambalo limeangalia maafa ya mafuriko yaliyotokea, Kilosa kwa mwaka 2014 na 2016, litatusaidia kuimarisha mifumo yetu serikalini ya kujiandaa na kukabili maafa ya mafuriko na majanga mengine kwani tumejua ni wapi hatukufanya vizuri na namna gani ya kuboresha mifumo yetu, lakini pia zoezi hili litawajengea uwezo waratibu wa maafa serikalini na wataalam kutoka katika mashirika yasiyokuwa ya serikali katika kushirikiana na serikali katika kujiandaa na kukabili maafa yatapotokea” Alisema Matamwe.
Aidha, washiriki wa zoezi hilo waliweza kutoa uzoefu wao katika kujiandaa na kukabili maafa ya mafuriko ambayo yalitokea wilayani Kilosa kwa mwaka 2014 na 2016. Washiriki hao kwa nyakati tofauti walibainisha kuwa wamejifunza kutoka mafuriko ya Kilosa kuwa ipo haja ya kila Serikali za mitaa na Taasisi za serikali pamoja na wadau wa menejimenti ya maafa kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya usimamizi wa shughuli za maafa.
Zoezi hilo lililofanyika kwa muda wa siku mbili tarehe 15 hadi 16, Julai, 2019, liliwashirikisha wataalam wa usimamizi wa shughuli za maafa kutoka serikalini na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali, limeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Social Plugin