Boti tano zenye silaha zinazoaminika kuwa za Jeshi la Iran zimejaribu leo kuimakamata meli ya mafuta ya Uingereza katika eneo la Ghuba bila mafanikio, Shirika la Utangazaji la CNN limeripoti likiwanukuu maafisa wawili wa Marekani wakisema, kuwa meli hiyo ya Uingereza ilikuwa ikiingia katika mlango bahari wa Hormuz wakati boti tano zilipoikaribia na kuiamuru kusimama katika mipaka ya bahari ya Iran.
Hata hivyo meli ya kivita ya Uingereza iliyokuwa ikiisindikiza meli hiyo ya mafuta ilitishia kuzishambulia boti za Iran na kuziamuru kuondoka.
Kisa hicho kinajiri siku chache tangu Uingereza ilipoikamata meli ya mafuta ya Iran katika eneo la Gibraltar kwa madai ya kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria.
Tukio hilo lilizusha mzozo mkubwa wa kidiplomasia kati ya Iran na Uingereza na Tehran ilitishia kuwa itakamata meli ya mafuta ya Uingereza kama hatua ya kulipa kisasi.