Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima akizungumza kwenye kikao cha madiwani
Na Dinna Maningo,Tarime.
Zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 zinadaiwa kuvuka mwaka pasipo kutumika katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime jambo linalodaiwa kukwamisha uendeshaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani kata ya Nyamwaga Misiwa Yomami kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime cha kujadili Taarifa ya mpango kazi na majibu ya Menejimenti kuhusu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni 30,2018.
Yomami alisema pamoja na Halmashauri hiyo kupata hati safi ,kuna fedha Bilioni 1.5 zimevuka mwaka bila kutumika kutokana na kucheleweshwa.
"Tunaomba Serikali itatue hii ni changamoto inayokwamisha utendaji pesa zote hizo zinavuka mwaka bila kutumika zingekuja kwa wakati zingesaidia kukamilisha masuala mbalimbali kwa wakati ,lakini pamoja na changamoto zinazojitokeza naipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi",alisema Yomami.
Akisoma Taarifa ya mpango kazi kuhusu hoja za Ukaguzi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Apoo Tindwa alitaja hati halmashauri ilizopata katika kipindi cha mwaka 2013-2018 ,ambapo mwaka 2013/2014 Halmashari ilipata Hati safi,2014/2015 Hati yenye shaka,2015/2016 Hati Safi,2016/2017 Hati safi na 2017/2018 Hati safi,na katika Miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha miaka hiyo imepata Hati safi ikiwemo miradi ya TASAF,ASDP, na HBF.
Tindwa aliongeza kuwa katika kutekeleza mkakati kwa ajili ya kuzuia hoja, kuna changamoto ambazo Halmashauri inahitaji kuzitatua ili kufikia lengo la kuondoa hoja ikiwemo fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida kutopokelewa kwa wakati kutoka hazina,tatizo la kukatika kwa mtandao wa mawasiliano na upungufu wa Watumishi katika Idara za Halmashauri.
Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima aliwataka Madiwani kushikamana ikiwa ni pamoja na kujadili,kuangalia mapungufu na kuzifanyia kazi hoja za CAG ili kusiwepo na hoja nyingi za ukaguzi.
January 2019 Halmashauri hiyo iliingia katika tuhuma nzito ambapo mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima akiongea na Madiwani aliihituhumu Halmashauri kwa matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo ambazo ni mapato ya ndani Bilioni 9.5 kutoka Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA uliopo Nyamongo tangu mwaka 2015-2018.
Malima aliunda Tume ya uchunguzi wa fedha hizo ikiongozwa na Katibu wake Mwita Chacha iliyoanza kazi Januari 28,2019 na kukamilisha uchunguzi Febuari 25,2019 na mwezi Aprili 2019 Tume hiyo mbele ya Madiwani na RC Malima ilieleza na kukiri uwepo wa ubadhilifu wa matumizi mabaya ya fedha ya Bilioni 15 kati ya hizo Bilioni 9.4 ni mapato ya Mgodi.
Kupitia tume hiyo aliiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa Takukuru kumchungunza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Apoo Tindwa huku Watumishi wengine 4 wakisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.
Social Plugin