Mbunge wa Geita mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema Halmashauri ya mji wa Geita hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu tayari imeshatoa mkopo wa Shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya wakinamama, vijana na walemavu kwa lengo la kutimiza adhima ya Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.
Amesema lengo la kutoa mkopo huo ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na kuweza kuinua kipato cha wananchi kwa kunufaika na miradi mbalimbali na hatimae kuweza kujikwamua kiuchumi.
Hayo ameyasema kwenye mkutano wakati akizungumza na wananchi wake kuhusu ahadi mbalimbali alizozitekeleza ikiwemo ya kutoa mkopo wa shilingi bilioni 1.6 kwa vikundi mbalimbali kwa lengo la kupunguza umasikini katika jamii katika mkutano huo uliofanyika katika kata ya Ihanamiro wilaya ya Geita mkoani Geita.
Mhe.Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa kutokana na uhusiano mzuri uliopo miongoni mwa madiwani katika Halmashauri hiyo wameweza kutoa mkopo huo. Hata hivyo amesema kuwa mikopo hiyo itasaidia katika uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kukuza uchumi
Akizungumza katika mkutano huo,Mhe.Kanyasu amesema anajisika fahali ya kutoa mikopo hiyo kwa vikundi ikiwa ni moja ahadi alizozitimiza za kuhakikisha mwananchi wake wanajihusisha kwenye shughuli za kiuchumi ili kupunguza umasikini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa
Amesema kuwa kutokana na changamoto zilizoko katika taasisi za fedha, ambazo hutoa mikopo kwa riba kubwa na kuhitaji dhamana ya nyumba na ardhi jambo ambalo linawakwamisha wakopaji hivyo serikali imeamua kutoa mikopo ya masharti nafuu.
Aidha amesema mikopo hiyo itawasaidia makundi hayo kuweza kuongeza mitaji na kutoa ajira ndani ya jamii.
Aidha, Mhe, Kanyasu amesema katika awamu ya pili ya utoaji mkopo wataongeza viwango vya mikopo kwenye vikundi ambapo kila kikundi kitakuwa na uwezo wa kukopeshwa hadi kufikia shilingi milioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Ihanamiro, Mhe. Joseph Lugaira amemueleza Mbunge huyo kuwa katika kata hiyo jumla ya vikundi 19 vimenufaika na mkopo huo kwa kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Amesema vikundi hivyo vimekuwa vikifanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara pamoja na kilimo ambapo anaamini wataweza kupata faida pamoja na kurejesha mkopo huo na kukopa tena.
Naye Diwani wa viti maalum, Mhe. Suzana Mashala amewahimiza wanawake wasiogope kukopa kwani hawawezi kujiendeleza kiuchumi pasipo kukopa.
Vile vile, Diwani huyo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanawake waliokopa wajitahidi kurejesha mikopo hiyo mapema ili mikopo hiyo iweze kuwasaidia watu wengine lengo likiwa ni kuondokana na umasikini.
Kwa upande wake, Emalio Nyangabo ambaye ni kiongozi wa Kikundi cha Tuinuane, amesema walipokea mkopo ambao umewasaidia kuinuka kiuchumi, na kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kuachana na kujihususha na vitendo visivyofaa katika jamii
Naye, Godson Maduka ambaye ni miongoni mwa vijana walionufaika wa mkopo huo amesema mkopo huo umewasaidia vijana wengi kujiepusha kujiingiza kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Social Plugin