Na Marco Maduhu - Malunde1 blog Shinyanga.
Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga amefanya ziara mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutatua changamoto ya zao la pamba kwa wakulima ikiwemo ununuaji wa zao hilo ili wakulima waweze kuuza na kupata fedha zao kwa wakati.
Hasunga ameanza ziara yake ya siku tatu mkoani hapa kuanzia leo Julai 15 na atakamilisha ziara hiyo Julai 17, 2019, ambapo ameanza kwa kutembelea wakulima wa zao la pamba, wamiliki wa viwanda wa zao hilo kwa ajili ya kuzungumza nao, na kuwatia moyo kuwa serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha changamoto zilizokuwa zinawakabili hapo awali zinatatuliwa.
Amesema Serikali inatambua changamoto iliyokuwepo awali ya kusuasua ununuzi wa zao hilo pamoja na wakulima kukopwa fedha za mauzo ya zao hilo kupitia kwenye vyama vya msingi vya ushirika AMCOS, lakini kwa sasa tatizo hilo limetatuliwa ambapo hadi kufikia Julai 30 mwaka huu wakulima wote watanunuliwa pamba yao pamoja na kulipwa fedha zao.
“Changamoto iliyojitokeza ni kuwepo kwa mgogoro kati ya nchi ya China na Marekani na kusababisha kushuka kwa dola, hali iliyopelekea bei ambayo tuliipanga ya mkulima kununuliwa pamba yake kwa shilingi 1,200 kuonekana kwa wafanyabiashara kutawatia hasara na hivyo kuacha kununua pamba,”amesema Hasunga.
“Lakini kwenye kikao ambacho tumekaa juzi na waziri mkuu Kasimu Majaliwa mkoani Tabora tumekubaliana kwamba kutokana na kushuka kwa dola, wafanyabiashara waendelee kununua pamba kwa bei hiyo ya 1,200, lakini dola ikiendelea kuwa chini basi serikali italipa fidia ya hasara ambayo wataipata, kuliko kushusha bei ya pamba ambayo itamuumiza mkulima,” ameongeza.
Pia amesema kutokana na kusuasua kwa masoko ya nje, serikali imejipanga kufufua viwanda vya ndani ambavyo huwa vinatumia malighafi ya zao hilo la pamba ili kuondoa changamoto hiyo ya kusu sua kwa ununuzi wa zao la pamba.
Katika hatua nyingine amewataka wakulima wa zao la pamba kujikita kulima kilimo chenye tija ambacho kitawapatia mavuno mengi, kuliko kuendelea kulima kwa mazoea na hatimaye kupata mavuno kidogo ambayo yatawapatia fedha kidogo na kushindwa kukua kiuchumi.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Albert Msovela akisoma taarifa ya mkoa huo, amesema kwa msimu wa kilimo (2018-19) zao la Pamba mkoani humo limelimwa hekta 97,270 na kutarajia kuvuna Tani 48,435, na kubainisha changamoto iliyopo kuwa ni ukosefu wa fedha ya kununulia pamba kwenye Vyama vya Msingi vya Ushirika AMCOS.
Nao baadhi ya wakulima wa zao la Pamba,akiwemo Peter Samson kutoka kijiji cha Mwaweja wilayani Kishapu, ambao ni miongoni mwa wakulima ambao wamekwenda kuuza pamba yao kwenye kiwanda cha Afrishan Shinyanga Mjini, wamesema wamekwenda kuuza pamba yao hapo kutokana na vyama vya msingi vya ushirika AMCOS kutokuwa na pesa ya kuwalipa na hivyo kuwa azimu kuingia gharama tena ya usafirishaji na kupongeza juhudi hizo za Serikali za kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Uzogole Shinyanga mjini Kulwa Chagu, amekiri kutokuwa na pesa ya kuwalipa wakulima pale wanaponunua pamba yao, na hivyo kushindwa kuendelea na zoezi la ununuaji wa pamba hiyo, ambapo kwa sasa wakulima wanaiuza kwenye kiwanda cha Afrishan ambacho ndiyo mkombozi wao.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga akizungumzia lengo la ziara yake mkoani Shinyanga kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack (kulia), kuwa ni kutatua changamoto zinazolikabili zao la Pamba likiwamo na suala la kusuasua kwa ununuzi wa zao hilo.Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
Awali Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Albert Msovela akisoma taarifa ya mkoa huo juu ya zao la pamba na kuelezea kuwepo na changamoto juu ya kusuasua kwa ununuaji wa zao hilo kwenye vyama vya Msingi vya Ushirika AMCOS kutokana na ukosefu wa fedha.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, akiipongeza Serikali kuitatua changamoto hiyo ya ununuaji wa zao la Pamba kwa wakulima.
Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad akipongeza jitihada za Serikali za utatuzi wa changamoto hiyo ya zao la Pamba, na kuomba pia lifanyiwe kazi suala la kuzuia wafanyabishara wa zao la dengu kutoinunua kwa wakulima hadi AMCOS jambo ambalo litasababisha kutokea kama kwenye kilimo cha pamba, ambapo waziri alifuta agizo la kuzuiwa wafanyabishara hao kutonunua zao hilo moja kwa moja kwa mkulima.
Waziri wa Kilimo.Mhe. Japhet Hasunga akiwasili kwenye kiwanda cha Afrishan Shinyanga Mjini ambacho kinanunua Pamba kutoka kwa wakulima licha ya wafanyabishara wengine kushindwa kuinunua Pamba hiyo kwa bei ya 1,200 mara baada ya kushuka kwa dola kwenye soko la nje kwa kuhofia ya kupata hasara.
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akiwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack (mwenye ushungi kichwani) pamoja na viongozi wengine wa mkoa huo, wakiangalia namna ununuaji wa Pamba unavyofanyika kwenye kiwanda hicho cha Afrishan kupitia vyama vya msingi vya ushirika AMCOS ambavyo na viwezeshwa fedha na kisha kuinunua kupitia kwao.
Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda cha Afrishan Shinyanga Mjini Ally Habshy, akizungumza ambapo amesema kwa sasa wananunua pamba hiyo kwa mkulima kwa bei ya shilingi 1,200 kupitia fedha zao za ndani, ambapo benki zilisuasua kuwapatia fedha na kupongeza jitihada hizo za Serikali za kutatua changamoto hiyo ya ununuzi wa zao la Pamba pamoja na wao wafanyabiashara kuwa watakopeshwa fedha za ununuaji wa pamba.
Ununuaji wa zao la pamba ukiendelea nje ya kiwanda cha Afrishan Shinyanga mjini.
Wakulima wakiendelea kuleta Pamba yao kuuzwa kwenye kiwanda hicho cha Afrishan Shinyanga mjini ambapo wengine wanatoka Igunga na Mwanza kwa ajili ya kuuza Pamba yao na kupata fedha taslimu.
Wakulima wakiendelea kuleta Pamba yao kuuzwa kwenye kiwanda hicho cha Afrishan Shinyanga mjini ambapo wengine wanatoka Igunga na Mwanza kwa ajili ya kuuza Pamba yao na kupata fedha taslimu.
Pamba ikiwa imemwagwa chini.
Wakulima wa zao la Pamba wakiwa kwenye kiwanda cha Afrishan Shinyanga Mjini wakiuza Pamba yao, mara baada ya vyama vya msingi vya ushirika AMCOS kukosa fedha ya kuwanunulia pamba hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwataka wakulima hao wa Pamba kutoiweka Pamba chini ambapo inachafuka bali waiweke sehemu ambapo ni pasafi chini ya matulubai na kutoipotezea ubora wake.
Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga akiwataka wakulima, kuwa wavumilivu wakati Serikali ikilitatua tatizo la ununuzi wa zao hilo ambapo hadi kufikia Julai 30 fedha zitakuwa zimepatikana na Pamba yote ya mkulima itanunuliwa pamoja na kulipwa pesa zao zote.
Wakulima wa Pamba wakisikiliza ujumbe kutoka serikalini juu ya utatuzi wa changamoto hiyo ya ununuzi wa zao la Pamba kupitia kwenye vyama vya msingi vya ushirika AMCOS.
Awali mkuu wa wilaya ya Shinyanga ,Mhe.Jasinta Mboneko mkono wa kulia akimkaribisha Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga alipowasili mkoani Shinyanga kwa ajili ya ziara ya siku tatu ya kutatua changamoto ya zao la pamba.
Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga akifurahia jambo na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko mkono wa kulia.
Waziri wa Kilimo,Mhe. Japhet Hasunga akifurahia jambo na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko mkono wa kulia.
Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
Social Plugin