Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa vikao vya kuchunguza tuhuma za ufisadi dhidi yake, ni njama iliyopangwa dhidi yake.
Zuma aliyasema hayo jana Jumatatu katika kikao cha uchunguzi wa faili la tuhuma za ufisadi wa fedha zinazomkabilia ambapo alikitaja kikao hicho kuwa ni njama dhidi yake.
Aliongeza kwamba maadui wake hata walipanga njama ya kutaka kumuua, kwa kuwa walikuwa wanataka kutwaa madaraka na kumuweka kando.
Mwanzoni mwa utetezi wake kwenye kikao hicho alisema kuwa tuhuma hizo zilikuwa na lengo la kumuondoa madarakani.
Itakumbukuwa kuwa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini aliondolewa madarakani mwezi Februari mwaka jana.
Aidha Zuma anatuhumiwa kwamba katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wake, aliwapa fursa watu wake wa karibu kutumia mali ya umma kwa maslahi yao binafsi na pia kuwateua katika nafasi mbalimbali serikalini.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini ametupilia mbali tuhuma hizo akizitaja kuwa ni za kisiasa tu.
Katika hatua za kuendelea kumbana Jacob Zuma katikati ya mwezi Agosti mwaka jana Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilibatilisha uteuzi wa Mwendesha Mashtaka Mkuu ambaye alipewa kazi na Jacob Zuma baada ya kumpiga kalamu nyekundu afisa aliyekuwepo kabla yake.
Kadhalika mahakama hiyo ilitoa amri kwamba, mwendesha mashtaka mkuu wa zamani arejeshwe kazini katika muda wa siku 90 kwa lengo la kufuatialia faili la tuhuma za ufisadi dhidi ya rais huyo wa zamani.
Social Plugin