Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema wanafanya uchunguzi wa sauti zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinazodaiwa ni za baadhi ya viongozi wa wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali.
Sauti hizo fupi za mazungumzo ya simu zinadaiwa kuwa za Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye; aliyekuwa waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba; makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba pamoja na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Benard Membe.
IGP Simon Sirro amesema wameziona sauti hizo na wameanza kuzifanyia uchunguzi japo hajafahamu uchunguzi huo utakamilika baada ya muda gani na endapo itathibitika kuna makosa ya jinai, watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria.
"Ni kweli hata sisi hizo sauti nimezisikia na tunafuatilia ili kujua ukweli wake, tukibaini kama kuna kesi ya jinai na kama yaliyokuwa yakitamkwa ni kweli basi tutachukua hatia za kisheria", amesema.
"Kuhusu uchunguzi utakuwa muda gani mimi sijui, inategemea shauri lenyewe", ameongeza IGP Sirro
Wakati huohuo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kupitia msemaji wake, Semu Mwakyanjala ameeleza kuwa suala hilo wamewaachia Jeshi la Polisi.
"Uhalifu wowote unaoripotiwa na TCRA watu wanaoshughulika na hilo ni Jeshi la Polisi, ila ninachosema kama kuna kosa la jinai, muhusika ashirikiane na Jeshi la Polisi ili ukweli ufahamike", amesema Mwakyanjala.