Jeshi la Polisi Latoa sababu za kumkamata mwandishi wa habari Erick Kabendera

Polisi kanda maalum ya Dar es salaam imethibitisha kumkamata mwandishi wa kujitegemea, Erick Kabendera kwa kutotii wito alioitwa na jeshi hilo. 

Polisi wamesema kuitwa kwake ni kutaka kutoa utata wa uraia wake na wanaendelea na uchunguzi na kumuhoji kama ni Mtanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 30, 2019, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema walimkamata jana Jumatatu Kabendera baada ya kupelekewa wito wa kufika polisi lakini akakaidi.

"Kuhusu taarifa za Mwanahabari Erick Kabendera ni kwamba July 29 tulimkamata nyumbani kwake baada ya kukataa wito wa Polisi, aliandikiwa barua ya wito kwa ajili ya mahojiano akakaidi, utii wa sheria bila shuruti ni muhimu sana ili kuzuia matokeo ya kukaidi wito halali.

"Sababu ya Erick kuitwa ni kuhusiana na utata wa Uraia wake, Polisi wanaendelea kupeleleza kwa kushirikiana na Uhamiaji ili kuhakikisha lile ambalo anatuhumiwa nalo linawekwa mezani ili athibitishe yeye ni Mtanzania kwa kutoa vielelezo mbalimbali.

"Kama Erick angefika alipoitwa angehojiwa na kuruhusiwa, lakini kwa kuwa ana mashaka ya uraia wake akakataa wito, sasa tuko nae na taratibu za upelelezi zinaendelea, hakutekwa, alikamatwa na wakamataji ni sisi na yuko salama.

"Baada ya kumkamata(Erick), kumezuka taarifa kutoka kwa kada mbalimbali kwenye jamii wengine Wanahabari wakiendelea kusema Mwandishi huyo ametekwa, wala hakutekwa aliitwa lakini kwa ujeuri akawa amekaidi wito huo"- Amesema Mambosasa





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post