MWANAHABARI AGNES KABIGI KUZIKWA KESHO DAR


Mwili wa aliyekuwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi kwa Watoto na Familia (Agpahi), Agnes Kabigi, aliyefariki dunia akiwa kazini wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga utazikwa kesho Jumanne Julai 30,2019 katika makaburi ya Bahari Beach kwa Kondo Goba, Dar es Salaam.


Agnes ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari mwandamizi alifariki dunia Ijumaa wiki iliyopita mchana baada kuanguka ghafla wakati akitekeleza majukumu yake akiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Mwili wake uliagwa juzi mkoani humo na kusafirishwa hadi jijini Dar es salaam kwa ajili ya maziko.

Katika uhai wake Agnes aliwahi kufanya kazi katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Nipashe na wakati mauti yanamkuta alikuwa anafanya kazi katika shirika la Agpahi ambalo linafanya shughuli zake katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika la Agpahi wakati wa kuaga mwili wa marehemu, mfanyakazi wa shirika hilo mkoa wa Shinyanga, Kasablankhahr Herman, alisema wakati wa uhai wake, Agnes alikuwa mfanyakazi mbunifu na mwenye uwezo wa hali ya juu hasa katika kutekeleza majukumu yake.

“Alikuwa ni mfanyakazi ambaye hakuna mtu aliyechoka kufanya naye kazi, alikuwa na uwezo wa kazi na aliipenda kazi yake, hakika ni pigo kubwa kwenye shirika na pia nitoe pole kwa tasnia ya wanahabari,” alisema.

Akizungumza na gazeti la Habarileo, mwanahabari, Beatrice Bandawe aliyewahi kufanya kazi na marehemu katika gazeti la Nipashe alisema Agnes alikuwa mchapakazi aliyeipenda kazi yake huku akiongozwa na misimamo dhabiti hasa katika kusimamia maadili ya kazi.

“Ninakumbuka mwaka 1996 ninajiunga na Nipashe, Agnes ndio alinipokea na alikuwa akinifundisha na kuniongoza katika kazi, hakika ni pigo kwa tasnia kwa kuondokewa na mkongwe mahiri katika fani kama huyu,” alisema.

Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post