Na. Edward Kondela
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeitaka Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) kubadilika na kufanya shughuli zake kwa tija ili iweze kunufaika na rasilimali ardhi na mifugo inayomiliki.
Akizungumza wakati akitembelea na kujionea shughuli zinazofanywa katika ranchi za Ruvu iliyopo Mkoani Pwani na Mkata iliyopo Mkoani Morogoro jana (01.07.2019), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amezitaka ranchi hizo zilizo chini ya NARCO kuhakikisha zinatumia vitu ardhi inazomiliki ili kufuga mifugo itakayoongeza tija kwa taifa.
Prof. Gariel akiwa katika Ranchi ya Ruvu amemuelekeza meneja wa ranchi hiyo Bw. Elisa Binamungu kuhakikisha ranchi hiyo inafuatilia pia madeni yote inayodai ili iweze kupata fedha na kujiendesha kwa kutumia fursa zilizopo za kuuza kwa tija mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa.
“Lengo la ziara yangu ni kuhakikisha mnatekeleza agizo alilolitoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina June 15 mwaka huu, alipokutana na viongozi wa NARCO la kuwataka kubadilika kiutendaji na muweze kunufaika na ardhi na mifugo mnayomiliki hali kadhalika kuweza kutoa gawio serikalini.” Alisema Prof. Gabriel.
Akiwa katika Ranchi ya Mkata Prof. Gabriel amejionea ujenzi wa kisima kwa ajili ya kupata maji ya kunyweshea mifugo na kumuagiza meneja wa ranchi hiyo Bw. Iddy Athuman kuhakikisha kisima hicho kinakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa kuwa ranchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya maji kwa mifugo.
“Ni muhimu kisima hiki kikamilike kwa kuwa maji ni uchumi mtakapokuwa na maji mengi ndivyo mtakavyoweza kuwa na mifugo kulingana na uwepo wa maji, pia kuhusu wazo lenu la kuanza kufuga ng’ombe wa maziwa ni wazo zuri hususan kisima hiki kikianza kutumika na kuwa na maji ya kutosha.” Alifafanua Prof. Gabriel.
Wakiwa katika ranchi wanazozisimamia mameneja hao wamesema watatekeleza maagizo yote kwa wakati kama yalivyoelekezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ili ranchi hizo za Ruvu na Mkata ziweze kunufaika kupitia rasilimali ardhi na mifugo zinazomiliki.
Social Plugin