Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RPC SHINYANGA - 'MSHIRIKI SHINDANO LA MISS SHINYANGA 2019 ALIPIGWA NGUMI,KUCHANIWA NGUO'


Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Richard Abwao

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limethibitisha taarifa za Mwanamitindo Nicole Emmanuel (19) kupigwa na waandaaji wa Mashindano ya Ulimbwende 'Miss Shinyanga 2019' baada ya mrembo huyo kudai gharama ambazo alitumia katika Shindano la Miss Shinyanga 2019.

Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumamosi Julai 13,2019 na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Richard Abwao, tukio hilo la shambulio la kudhuru mwili limetokea Alhamis Julai 11,2019 majira ya 12 jioni katika maeneo ya Nedman hotel iliyopo Tambuka reli katika Manispaa ya Shinyanga.

"Mlalamikaji aitwaye Nicole d/o Emanuel (19),Mwanamitindo, Mkazi wa Dar es salaam, alishambuliwa kwa kupigwa ngumi, mateke na kuburuzwa chini kisha kuchaniwa nguo na kusababishiwa maumivu mwilini na watuhumiwa waliotajwa kuwa ni Mkurugenzi Richard Luhende na Meneja aliyetajwa kwa jina moja la George wote  wa Makumbusho Intertainment",ameeleza Kamanda Abwao.

"Tukio hilo limetokea baada ya mlalamikaji kuwadai watuhumiwa nauli na gharama ambazo alitumia katika Shindano la Miss Shinyanga 2019. Watuhumiwa wawili waliotajwa kuhusika katika tukio hili ni Mkurugenzina Meneja wote wa Makumbusho Intertainment ",amesema Kamanda Abwao. 

 "Shauri hili limeshafunguliwa na jitihada za kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa zimefanyika, na jioni hii ya leo tayari huyu Meneja George kakamatwa,yuko mikononi mwa polisi,taratibu za kipolisi zitaendelea kufuatwa ikiwemo kulifikisha shauri hili mahakamani",amesema Kamanda Abwao.

Awali siku ya Alhamis akizungumza na waandishi wa habari Nicole Emmanuel alisema alifikwa na majanga hayo wakati akidai fedha zake nauli shilingi 70,000/= ili arudi Dar es salaam.

Nicole aliwataja waandaji wa Shindano hilo waliompiga kuwa ni Meneja Mkuu wa Makumbusho Entertainment,George Foda na Mkurugenzi wa Makumbusho Entertainment Richard Luhende.

Hata hivyo Meneja Mkuu Makumbusho Entertainment George Foda,aliyekuwa anasimamia mashindano ya Miss Shinyanga 2019 ,alikanusha taarifa za kumpiga mrembo huyo huku akikiri kwamba ni kweli mrembo huyo alikuwa anawadai pesa na katika kudai pesa hizo alianza kuleta fujo hotelini kutumia lugha chafu na kugonga geti ndipo wakamchukua na kumpeleka kituo cha polisi.

Na Kadama Malunde -Malunde1 blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com