Watu wasiopungua saba wanaripotiwa kuuawa nchini Sudan baada ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kutumia mkono wa chuma kuyatawanya maandamano ya wananchi ya kutaka utawala wa kiraia.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, maandamano makubwa ya jana ya wananchi wa Sudan katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum yaligeuka kuwa umwagaji damu baada ya vikosi vya usalama kuwavamia waandamanaji na kuwafyatulia risasi.
Wananchi hao walikuwa wakishiriki katika maandamano ya kutoa wito kwa Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo kukabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Duru za hospitali zinasema kuwa, watu karibu mia mbili wamejeruhiwa.
Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Omar Hassan al-Bashir.
Tangu Hapo, wananchi walianza kuandamana tena wakilitaka Jeshi likabidhi Madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Social Plugin