Rais Magufuli ameeleza sababu za kumrejesha kazini Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James Mataragio, aliyesimamishwa kazi mwaka 2016.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa kupokea vipande 22 vya dhahabu vyenye uzito wa kilo 35.34 na fedha zilizodaiwa kuibwa nchini mwaka 2004 katika Benki ya NBC Moshi mkoani Kilimanjaro, Rais Magufuli alifichua mchezo mchafu uliofanywa dhidi ya kigogo huyo.
Alisema mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi baada ya kupinga kuuzwa kwa vitalu vyote vya gesi na Tanzania kubaki bila kitalu hata kimoja inachomiliki.
"Huyu mkurugenzi alisimamishwa kazi baada ya kukataa rushwa ya kampuni fulani iliyokuwa inataka vitalu baharini. Alipigania tubaki na vitalu viwili, tuwekeze fedha kidogo kidogo na kuchimba wenyewe kuliko kuwapa vyote wawekezaji," alibainisha Rais Magufuli.
Jumatatu wiki hii, Ikulu ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwa Rais Magufuli ameagiza kurejeshwa kazini kwa mkurugenzi huyo mara moja.
Mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC Agosti 20, mwaka 2016 na Rais amebatilisha uamuzi huo na kumwagiza Waziri wa Nishati kumrejesha kazini haraka.
Social Plugin