Mtu mmoja amepoteza maisha yake huku waumini wengine wachache na mapasta wao wakiuguza majeraha baada ya Majambazi kuvamia kanisa la Shekinah Pentecostal lililopo jijini Nairobi nchini Kenya wakati wa maombi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio hao waliingia katika kanisa hilo na kuwavamia waumini akiwemo pasta wa kanisa hilo leo Ijumaa, Julai 12,2019 asubuhi.
Majambazi hao wanakisiwa kutoweka na kiasi cha pesa zisizojulikana pamoja na vyombo vingine vya kanisa.
Mashahidi wameeleza kuwa marehemu alikuwa anajipitia zake wakati alipodungwa kisu na genge hilo nje ya kanisa baada ya kutekeleza uhalifu wao na kujaribu kutoroka.
‘‘Ilikuwa mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, majambazi hawa wakavamia kanisa na kuwadunga visu waumini ambao walikuwa wamekutana kwa maombi ya asubuhi kabla ya kumuua mwanaume mmoja ambaye alikuwa tu mpita njia kwa kumdunga kisu na kisha wakatoroka walinzi wa kanisa walipokuwa wakijaribu kuwafuata," alisema shahidi huyo.
Wakazi wa mtaaa huo wanawaomba maafisa wa polisi wa Makongeni kufanya uchunguzi wa haraka na kuwakamata wahalifu hao waliotekeleza kisa hicho cha kinyama.
Kufikia sasa walinzi wa kanisa hilo wameandikisha taarifa katika kituo cha polisi huku waathiriwa wakiendelea kupokea matibabu.
Taarifa yake J.Papanoo, Mwandishi wa TUKO.co.ke kaunti ya Nairobi
Social Plugin