Mnada wa kuuza Vifaa na samani mbalimbali vya Kampuni ya Mbowe Limited, inayomilikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, umeonekana kufanikiwa kwa kiasi baada ya baadhi ya vifaa hivyo kununuliwa na kusalia vichache.
Mnada huo ulioendeshwa na Kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneer & General Traders ya Dar Es Salaam, umefanyika leo Julai 6, 2019 chini ya dalali wa mahakama Joshua Mwaituka, kwenye ghala la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo maeneo ya Bandari.
Akizungumza kuhusu mnada huo, Mwaituka amesema mwitikio wa wateja umekuwa ni mzuri na kwamba asilimia kubwa ya vifaa hivyo vimepata wateja,ambapo amevitaja vifaa vilivyonunuliwa ikiwa ni pamoja na taa, jukwaa, viti, kreti za bia, genereta,Mashine za kupozea na samani mbalimbali.
''Vitu vyote vimeuzwa kasoro makochi, na bei zake ni za kawaida na mwitikio wa watu ni mzuri wamefika tangu saa 2:00 asubuhi''
Kwa upande wake Meneja wa ukusanyaji Madeni kutoka NHC amesema mnada huo ni mwendelezo wa shirika hilo katika kudai deni la zaidi ya shilingi bilioni 1 na kwamba fedha zitakazopatikana kupitia mnada huo, zitaingizwa katika deni la kampuni hiyo na kiasi cha deni kitakachosalia wahusika watalipa kwa mujibu wa sheria.
Vifaa vilivyopigwa mnada vilikuwa vikitumika katika klabu ya Bilicanas, vilichukuliwa na NHC Septemba mwaka 2016, baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa deni la zaidi ya shilingi bilioni 1 alilokuwa anadaiwa kwa kutokulipa kodi kwa muda wa miaka 20.