Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ametoa tahadhali kwa Serikali akishauri hatua kadhaa zifanyike kabla ya kufanyika mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo utafanyika Tanzania Agosti 17 na 18 mwaka 2019 ukitanguliwa na mikutano mbalimbali pamoja na Maonyesho ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za SADC chini ya kauli mbiu ya Mazingira Wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda.
Katika hotuba yake wakati wa Mkutano Mkuu wa NCCR Mageuzi kwa ajili ya kuchagua viongozi wapya wa chama hicho jana Jumamosi Julai 27,2019, Mbati ambaye ni Mbunge wa Vunjo aliitaka Serikali ifanye uchambuzi kwa kuangalia uamuzi wake katika maeneo mbalimbali yanayoonekana kuwa kikwazo katika mtangamano huo.
“Tanzania ni sehemu nzuri ya kujenga ubia, mazingira mazuri ya kibiashara lakini Serikali yetu waangalie namna ya kufanya uamuzi katika masuala ya kikodi, mifumo endelevu ya kikodi, kodi zinazotabirika, mazingira rafiki ya uwekezaji, mazingira ya kuvutia, mazingira yasiyo na vikwazo ili kuchochea ukuaji wa uchumi kulingana na kasi ya mabadiliko ya Kiuchumi duniani,” alisema Mbatia.
“Wakubali au wakatae, hata wangefunga masikio yao, sekta binafsi ndiyo msingi wa uchumi wa Taifa, huo ndiyo ukweli wa leo, tuwajenge mazingira rafiki, tusiwabeze.”