MBUNGE WA NJOMBE AWAFUNGUA WAJASIRIAMALI JUU YA BENKI YA KILIMO

Na Amiri kilagalila-Njombe

Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini kupitia chama cha mapinduzi (CCM), Edward Mwalongo amekutana na kufanya mazungumzo na Wadau wa Kilimo Mjini Njombe juu ya kutumia fursa za masoko ya kilimo ya ndani na nje ya Tanzania.

Mwalongo Amesema kuwa Wajasiriamali hao wanatakiwa kutumia fursa zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuomba mikopo ili kuongeza thamani ya shughuli zao za Kilimo badala ya kukaa na kulalamika kuwa hawana mitaji.

“Lengo kubwa la kukutana na hawa Wajasiriamali wadogo wadogo wa Jimbo la Njombe Mjini, ni kuwakumbusha namna bora ya kutafuta na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi yetu ikiwemo kupeleka nafaka nchi jirani ya Congo,” amesema Mwalongo.

Aidha, amewataka Wajasiriamali hao kuwa na umoja na mshikamano katika kufanya shughuli zao za Kilimo, ikiwa pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika na kuchakata nafaka ili waingize sokoni kwa haraka.

Salum Sanga na Clemence Malekela ni baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta ya viwanda vya kuchakata unga ambao wanasema bado wameendelea kukabiliwa na changamoto ya watalaamu wa halmashauri kugoma kutoa vibali vya kujenga viwanda pamoja na maeneo tengwa ya viwanda.

Wakizungumzia kuhusu soko wawekezaji hao wa ndani ya mkoa wa Njombe wanakiri kwamba zaidi ya miaka mitatu wakulima wameshindwa kuuza mahindi kutokana na kuporomoka kwa soko na kwamba kitendo cha mbunge huyo kwa kushirikiana na serikali kufungua masoko ya nje ya nchi kama Zambia , Kenya na Congo itasaidia kukata kiu yao.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post