Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amewataka viongozi wa dini, serikali na wastaafu kukemea suala la utekaji kwani haiwezekani watu kuishi nchini kwa wasiwasi.
Amezungumza hayo leo na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati alipokuja kusikiliza kesi ya madai aliyofungua dhidi ya mmiliki wa gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba na wachapishaji wa gazeti hilo.
“Huu ni utamaduni mpya ambao haukubaliki na ningependa kuchukua nafasi hii kusema kwamba suala la utekaji na watu kupotea linaweza kuiondolea nchi yetu heshima duniani tangu tupate uhuru, hivyo ningependa kuwaomba viongozi wote walikemee,”
“Viongozi wa serikali wasione aibu hata wa Dini wasiogope na wastaafu wote lazima tukemee utamaduni huu mpya, hatuwezi kuendelea kuishi katika nchi yenye watu wenye wasiwasi na uoga ambao hawajui kesho wataamka vipi na hii ajenda iishe maana isipo isha itaenda kwenye uchaguzi mwakani,” Membe
Aidha, akizungumzia kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kupoteza ubunge, Membe amesema kama Mtanzania ameshangaa sana.
“Mimi kama Mtanzania nilishangazwa sana na uamuzi wa Spika, Job Ndugai lakini tusubiri Lissu arudi.
“Nina uhakika atakwenda mahakamani kudai haki yake na kama ipo haki ataipata mahakamani,” amesema Membe
Social Plugin