Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIKANDA MIWILI YA VIDEO YENYE USHAHIDI YAWASILISHWA KESI YA FREEMAN MBOWE NA VIGOGO WENGINE CHADEMA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepokea kielelezo cha Kamera ya kurekodia video na tepu mbili kwa ajili ya kutumika katika ushahidi wa kesi ya uchochezi inayowakabili Viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe.


Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Hakimu Simba amesema kuwa Kifungu cha 18 cha sheria ya ushahidi wa kieletroniki kimeweka vigezo vya upokeaji wa vielelezo vya eletroniki ambavyo shahidi namba sita Koplo Charles alikidhi.

Kielelezo hicho kilitolewa na shahidi wa sita katika kesi hiyo, Koplo Charles.

Alidai saa 10 alasiri watu walianza kukusanyika katika Uwanja wa Buibui na mshereheshaji alitangaza kwamba viongozi wakuu wa chama wameshafika na baada ya muda wabunge na viongozi wakuu walipanda jukwaani na alimsikia Mbowe akitoa kauli za kufanya hamasa ya kuichukia Serikali.

Koplo Charles aliomba kutoa vifaa hivyo kama kielelezo, upande wa utetezi walipinga, lakini katika uamuzi wa mahakama vielelezo hivyo vimepokewa.

Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu, Vicent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa – Zanzibar, Salimu Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com