Mabingwa watetezi Cameroon na wenyeji Misri wameyaaga mashindano Jumamosi Juni 6 baada ya kutolewa kwenye siku ya pili ya hatua ya mtoano.
Cameroon na Misri ndio waliocheza fainali ya Kombe la Maifa ya Afrika (Afcon) miaka miwili iliyopita ambapo Cameroon ilitwaa ubingwa.
Hata hivyo timu hizo mbili zimeyaaga mashindano baada ya Cameroon kufungwa 3-2 dhidi ya Nigeria jijini Alexandria.
Misri wamepigwa mbele ya mashabiki elfu sabini jijini Cairo na Afrika Kusini kwa goli moja tu lililofungwa na Thembinkosi Lorch katika dakika ya 85.
Afrika Kusini ambao walifuzu katika raundi ya mtoano kama timu ya tatu kwenye kundi lao baada ya kushinda mchezo mmoja tu haikupigiwa upatu katika mechi ya hiyo dhidi ya Misri inayoongozwa na mshambuliaji wa Liverpool Mo Salah.
Umakini wa safu ya ulinzi wa Afrika Kusini ndio imekuwa chachu ya ushindi baada ya kuhimili vishindo na mikiki ya safu ya ushambuliaji ya Misri ambayo iliibuka na ushindi kwenye mechi zote tatu za makundi.