Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MISS ARUSHA 2019 AKABIDHIWA ZAWADI YA KIWANJA CHA SHILINGI MILIONI 6

Na Eliya Mbonea-Arusha
MREMBO Gladness Kaaya aliyetwaa taji la Miss Arusha 2019 hatimaye amekabidhiwa rasmi zawadi yake ya Kiwanja chenye thamani ya Sh milioni sita.

Kiwanja hicho kilichopo eneo la Njiro mjini Arusha kimetolewa na wadhamini wa mashindano hayo Kampuni ya Kambele Investment wauzaji wa viwanja.

Akizungumza kwenye makabidhiano ya kiwanja hicho Mkurugenzi wa Kambele, Weson Kambele amesema, wametoa kiwanja chenye thamani ya Sh milioni sita kwa mrembo huyo ili kumpa nafasi ya kuanza maisha.

“Tungeweza kutoa zawadi nyingine, lakini mtakubaliana nasi kwamba maisha ni nyumba, tunaamini atakuwa na fursa pana sasa ya kuanza kufikiri ajenge nyumba gani kwanja tayari anacho,” amesema Kambele.

Kwa upande wake Meneja wa Itifaki wa kampuni ya The Function House iliyoandaa mashindano hayo Basil Elias alimtaka Miss Arusha kutumia fursa hiyo kujiendeleza kimaisha pamoja na masomo.

“Mrembo wetu amekabidhiwa zawadi tuliyomuahidi naamini atakuwa na muda mzuri wa kusoma, kujiendeleza kimaisha kwani tayari amepunguza jambo muhimu la kuwa na kiwanja,” alisema Basil na kuongeza:

“Tunaamini atafanya vizuri katika ngazi zinazofuata na tumemuomba ahakikishe anakuwa balozi mzuri wa kutangaza utalii na vivutio vya utalii vinavyopatikana mkoani Arusha,” amesema.

Naye Miss Arusha Gladness Kaaya ameshukuru kwa kukabidhiwa zawadi hiyo ya kiwanja na kuwahidi kwamba atakiendeleza kwa kujenga mjengo wa kisasa ili iwe mfano kwa wasichana wengine.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com