Na Marco Maduhu na Kadama Malunde -Malunde1 blog.
Mshiriki wa mashindano ya ulimbwende mkoani Shinyanga (Miss Shinyanga 2019) Nicole Emmanuel, amedai kupigwa na kuchaniwa nguo hadharani na waandaji wa mashindano hayo wa Kampuni ya Burudani ya Makumbusho Entertainment mjini Shinyanga wakati akidai fedha zake nauli shilingi 70,000/=.
Tukio hilo limetokea jana Julai 11,2019 majira ya saa 11 jioni kwenye hotel ya Nedman iliyopo ushirika Shinyanga mjini Miss huyo akiwa na mshiriki mwenzake wa shindano hilo aitwaye Agnes Masunga walipofika kwenye hoteli hiyo(kambi waliyokuwa wanaitumia) ili kudai nauli zao.
Waandaji wa Shindano hilo wanaotuhumiwa kumpiga na kumdhalilisha binti huyo ni Meneja Mkuu wa Makumbusho Entertainment,George Foda na Mkurugenzi wa Makumbusho Entertainment Richard Luhende ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari Miss huyo Nicole, alisema wakati wakiwa kwenye ushiriki wa mashindano hayo ya Miss Shinyanga ambayo yalifanyika Julai 6 mwaka huu, waliahidiwa kuwa kuanzia mshindi wa nafasi ya 4 hadi 13 watapewa kifuta jasho cha Shilingi 50,000 pamoja na nauli ya kurudi kwao lakini kwake hali ikawa tofauti.
“Baada ya mashindano kuisha na mimi sikubahatika kushinda Taji hilo la U miss Shinyanga,sikuingia kwenye tano bora, ikabidi niombe fedha zangu za nauli jumla shilingi 70,000 ili nirudi Dar es salaam nilikokuwa lakini nikaanza kuzungushwa pamoja na SMS za kutakwa kimapenzi,”alisema mrembo huyo.
“Leo mimi na mwenzangu Agnes Masunga tulienda Nedman kufuata nauli zetu,nikamuomba Meneja George anipe pesa zangu akasema Mkurugenzi hajaafiki mimi kupewa nauli,nikamwambia basi mimi naenda polisi kudai haki yangu,nikatoka,nilipofika getini nikamwambia bodaboda awashe pikipiki tuondoke ndipo George na Luhende wakanifuata na kuanza kunipiga vibao,ngumi,kunichania nguo ,kuniburuza chini,kunivuta nywele kunikaba shingo na kisha kunipeleka polisi wakidai nimefanya vurugu,”aliongeza.
"Wamenipeleka kituoni nguo zikiwa zimechanwa, kwenye gari alikuwemo Richard Luhende na George Foda wameenda kusingizia polisi kuwa mimi nimefanya vurugu wakati mimi nadai haki yangu,walikuwa wananitisha kuwa wao wana hela na madaraka watanifanyia kitu kibaya sitakaa nisahau katika maisha yangu..wamenipiga wameniumiza jicho la kushoto,mguuni nina jeraha,bega linauma baada ya kuruburuzwa chini,kichwa kinauma kwa kuvutwa nywele",alieleza.
"Nilivyofika kituoni Luhende akasema niwekwe ndani na kwamba atawapigia simu polisi baadae,akaja askari kunisikiliza baadaye akaja Mkuu wa kituo cha polisi ndiyo akawa amenisaidia pale,akawa anawauliza kwanini wamenifanya vile,nikamhadithia na mimi kile kilichotokea,ikaishia pale ndipo Luhende akanipa Shilingi 100,000 ili niondoke kituoni,lakini hakunipa gharama zozote za matibabu",alifafanua Mrembo huyo.
Kwa upande wake,Mwendesha bodaboda Japhet Kazimili aliyeshuhudia tukio la mrembo huyo kupigwa alisema akiwa getini alishuhudia Nicole akipigwa mtama na kuchaniwa nguo kisha kuwekwa ndani ya gari na George na Luhende huku dada huyo akilia akiomba msaada.
Hata hivyo meneja mkuu Makumbusho Entertainment George Foda, licha ya kudai waandishi wa habari wamekurupuka,alikanusha kumtembezea kichapo Miss huyo huku akikiri kwamba ni kweli mrembo huyo alikuwa anawadai pesa na katika kudai pesa hizo alianza kuleta fujo hotelini ndipo wakamchukua na kumpeleka kituo cha polisi.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Abwao amesema binti huyo hajafungua kesi na kama atafungua kesi polisi watampa ushirikiano.
Aidha Mama mlezi wa binti huyo Grace Elias ambaye pia ni mama mzazi wa Agnes Masunga ambaye naye alikuwa akidai fedha yake, alilaani kitendo hicho cha waandaji wamashindano hayo ya Miss Shinyanga kuwafanyia ukatili wa kijisia watoto hao kwa kuwadhalilisha kingono pamoja na kuwapiga pale wanapodai haki zao.
Grace Elias alisema binti yake amekaa kambini siku 15 na akiwa kambini alipoteza simu yake ya shilingi 270,000/= lakini waandaji wa shindano hilo hawakutoa ushirikiano ili simu ipatikane lakini pia binti yake pia hakuingia kwenye tano naye hakupewa kifuta jasho chake na baada ya kusumbuana nao sana ndiyo amepewa shilingi 50,000/- baada ya kufikishana polisi.
Kampuni ya Makumbusho Entertainment pia ni Waandaaji wa Shindano la Miss Lake Zone linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni Mkoani Shinyanga.
Social Plugin