Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema amemaliza muda wake wa kuongoza bodi hiyo.
Mrema aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuongoza bodi hiyo Julai16, 2016, jana Julai 16, 2019 ametimiza kipindi cha miaka mitatu cha kuongoza bodi hiyo.
Mrema ametangaza kumaliza muda wake jana nyumbani kwake Salasala, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari kuhusu utendaji wa bodi hiyo katika kipindi hicho ambapo ameiomba Serikali kuiongezea fedha za uendeshaji wa shughuli zake Bodi hiyo ili iweze kukidhi mahitaji ya utendaji wa kazi wa mikoa na Taifa kwa sababu fedha zinazotengwa na bajeti hazitoshelezi katika utendaji wa kazi zao.
Aidha, amemshauri Waziri wa Mambo ya Ndani, kuyafanyia kazi majalada yanayowasilishwa na bodi hiyo kutoka magereza mbalimbali kwani bila kufanya hivyo baadhi ya wafungwa wanaotakiwa kunufaika kumaliza vifungo wakiwa ndani.
Pia ameomba vyama visivyo vya kiserikali, taasisi mbali mbali na watu wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuwarekebisha wafungwa na kusaidia bodi za parole ili wafungwa wanapoachiwa huru na kurudi kwenye familia zao wawe wamerekebeshika.
Mrema amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kumpa nafasi hiyo, akisema katika miaka mitatu wafungwa 742 kati yao 720 walipendekezwa na 648 waliachiliwa kwa msamaha wa Parole.
Amesema, wafungwa wote walioachiliwa kwa mpango wa Parole hakuna hata mmoja aliyevunja masharti na kurudishwa gerezani, kujihusisha au kuhusishwa na vitendo vya uhalifu.
Social Plugin