WAHUNI WAMTAPELI MWALIMU MSTAAFU MILIONI 60 ZA MAFAO


Mwalimu mstaafu mkazi wa Kiberege wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ametapeliwa pesa taslimu Sh60 milioni ambazo ni fedha za mafao na watu watatu waliojitambulisha kwake ni wafanyabiashara wa madini ya dhahabu.


Watu hao walidai kuwa soko lao lipo kwa mapadri wa kanisa la Mtakatifu Patrick mjini Morogoro.

Matapeli hao walikutana na mstaafu huyo Julai 20 mwaka 2019 maeneo ya Benki ya NMB tawi la Ifakara na kumtaka wafanye biashara ya madini ya dhahabu na baadaye waliondoka naye hadi mjini Morogoro kwa ajili ya kufanya makubaliano ya biashara hiyo.

Akizungumzia tukio hilo jana Ijumaa Julai 26,2019, kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa aliwataja watuhumiwa hao ni Shabii Rajabu, Mnyakile Luoga na Maulid Msiku aliyejitambulisha ni mhasibu wa kanisa la St. Patric jambo ambalo sio kweli.

Kamanda huyo alisema baada ya kufika mjini Morogoro mstaafu huyo alikwenda na matapeli hao benki ya NMB na kutoa pesa katika akaunti yake kiasi cha Sh60 milioni na kuwakabidhi matapeli hao na kumpatia madini ya dhahabu feki yakiwa kwenye maboksi madogo matatu yaliyokuwa yamezungushiwa utepe mweusi.

Alisema baada ya kupata kiasi hicho cha fedha matapeli hao waliokuwa na gari ndogo aina ya Noah walimshusha mstaafu huyo kwenye gari na kutoweka kusikojulikana.

Kamanda Mutafungwa alisema baada ya mstaafu huyo kufungua maboksi hayo alikutana na gololi za baiskeli na sio madini ya dhahabu hivyo alitoa taarifa kituo cha polisi Morogoro kuwa ametapeliwa na upelelezi ulianza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja anayeitwa Shabii Rajabu mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam.

Na Hamida Shariff, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post