Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai ameonesha kufurahishwa na utendaji kazi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi.
‘Utendaji wako wa kazi ni wa kiwango cha juu, tunaona mafanikio ya TMA katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa nchini kwa usahihi zaidi kulinganisha na huko nyuma ’ Alizungumza mhe. Ndugai
Mhe. Ndugai aliendelea kwa kumpongeza Dkt. Kijazi kwa kuchaguliwa kuwa makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwani imeonesha kazi kubwa inayofanywa na TMA chini ya uongozi wake hivyo kumpa nafasi ya kushinda kwa kishindo na kuiletea sifa nchi katika nyanja za kimataifa.
Katika hatua nyingine, wabunge wa Bunge la JMT walimpongeza Dkt. Kijazi kwa shangwe kubwa mara alipotambulishwa ndani ya Bunge hilo na Mhe. Spika kama makamu wa tatu wa Rais wa WMO.
Wabunge walionekana wakishangilia kwa furaha kuashiria kukubaliana na pongezi zilizokuwa zinawasilishwa na mhe. spika kwa niaba ya wabunge wote kabla ya kuahirisha rasmi vikao vya bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20
Naye, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipata wasaa wa kuliambia Bunge jinsi mchakato wa uchaguzi ulivyoenda na umuhimu wa nafasi hiyo ya juu kwa TMA, Tanzania na Afrika, sambamba na kulishukuru Bunge kwa ushirikiano waliouonesha katika kampeni za awali wakiwakilishwa na Mhe. Mboni Mhita , mbunge wa Handeni Vijijini.
Dkt. Kijazi alikutana na Mhe. Spika na kuhudhuria Bunge kupitia mwaliko wa Mhe. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano uliokuwa na lengo la kumtambulisha mteule wa nafasi ya makamu watatu wa Rais wa WMO kutoka Tanzania na kutoa shukrani za ushirikiano wa Bunge hilo.
Aidha, Dkt. Kijazi alimshukuru Mhe. Spika kwa pongezi na kuahidi kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu ya TMA na WMO ili kuendelea kuiletea heshima nchi katika sekta ya hali ya hewa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)
(Picha kwa hisani ya Ofisi ya Bunge)
Social Plugin