Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida utakaofanyika Julai 31, mwaka huu.
Akitangaza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage amesema ratiba inatokana na barua ya Spika inayoeleza kuwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu amepoteza sifa ya kuwa Mbunge kutokana na kushindwa kuwasilisha kwa Spika tamko la mali na madeni na kushindwa kuhudhuria mikutano saba mfululizo bila ruhusa ya Spika.
“Tumezingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki,” amesema.
Jaji Kaijage amesema, fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Julai 13 hadi 18 mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18, na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 na siku ya uchaguzi itakuwa ni Julai 31, mwaka huu.