Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO KATA 13 ZA TANZANIA BARA


Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Kata 13 ambao utafanyika tarehe 17 Agosti 2019.
Taarifa kwa umma iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (Rufaa) Mbarouk Salim Mbarouk Mjini Babati, Mkoani Manyara leo (tarehe 24.07.2019) imesema kwamba fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya tarehe 29 Julai mpaka tarehe 03 Agosti 2019.


Jaji Mbarouk amesema kwamba uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 03 Agosti 2019 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 04 Agosti 2019 mpaka tarehe 16 Agosti 2019.


Alizitaja kata zenye uchaguzi na halmashauri zake kwenye mabano kwamba ni pamoja na Laroi, Lemanyata na Likiding’a (Wilaya ya Arusha), Kimokouwa (Wilaya ya Longido), Kwembe (Manispaa ya Ubungo), Izigo (Wilaya ya Muleba), Mahida (Wilaya ya Rombo).


Nyingine ni pamoja na Makanya (Wilaya ya Same), Barikiwa (Wilaya ya Liwale), Kikeo (Wilaya ya Mvomero), Biro (Wilaya ya Malinyi), Myangayanga (Mji wa Mbinga) na Kapenta (Wilaya ya Sumbawanga).


Jaji Mbarouk amesema Tume imetangaza nafasi hizo kuwa wazi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, ameitaarifu Tume  uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata Kumi na tatu (13) zilizopo katika Halmashauri Kumi na moja  (11) na Mikoa Nane (8) ya Tanzania Bara.


Amesema nafasi wazi za udiwani katika Kata hizo zimetokana na sababu mbalimbali zikiwemo Vifo, Kujiuzulu na Uamuzi wa Mahakama.


“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Tume ina utaarifu Umma kuhusu kuwepo kwa Uchaguzi mdogo katika Kata hizo Kumi na tatu (13),” Jaji Mbarouk alisema.


Kwa taarifa hiyo, Jaji Mbarouk amesema Tume inavialika Vyama vya Siasa, Wadau wote wa Uchaguzi na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.


“Tume inachukua fursa hii kuviasa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi mdogo,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com