Mlinzi wa kati wa timu ya Yanga Abdallah Haji Shaibu (Ninja) amejiunga na timu ya MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech barani Ulaya kwa mkataba wa miaka 4.
Timu hiyo ambayo inashiriki ligi Daraja la Tatu nchini humo imepanga kumtoa kwa mkopo kwenda kucheza kwenye klabu ya LA Galaxy ambayo inashiriki ligi kuu Soka ya Marekani (MSL) ikiwa na nyota kadhaa waliyowika Duniani akiwemo mchezaji wa zamani wa Barcelona, Inter Milan na Manchester United Zlatan Ibrahimovic.
Meneja wa Mchezaji huyo Abubakar Khatib Kisandu amesema tayari wameshamalizana na MFK Vyskov ambayo inashiriki ligi Daraja la Tatu Jamhuri ya Czech ambapo atakwenda kwa mkopo Marekani kucheza LA Galaxy.
Alipoulizwa kuhusu dili hilo limekujaje Meneja Kisandu amesema kuna Kampuni ya Mawakala wa Wachezaji DreamWorld Sports and Entertainment LLC Player ndio iliyomuona Mlinzi huyo kwenye Michezo ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa mwaka 2017-2018 akiitumikia Yanga kwa mara ya kwanza na kufunga nao Mkataba ndipo ilipoamua kumpeleka Barani Ulaya.
Ninja alijiunga na Yanga June 14, 2017 kwa mkataba wa miaka 2 ambapo baada ya kumalizika mkataba wake mwaka huu ndipo alipoamua kwenda kucheza Soka Barani Ulaya.
Social Plugin