NA AVITUS BENEDICTO KYARUZI , KAGERA
Onyo imetolewa kwa Viongozi wanaotoza pesa wafanyabiashara wenye vitambulisho vilivyotolewa na Rais Magufuli kuacha vitendo hivyo mara moja.
Maagizo hayo yametolewa julai 11 mwaka huu na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli wakati akiwahutubia wananchi katika eneo la Rwamishenyi lililopo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wakati akiendelea na ziara yake mkoani hapa.
“Mimi ninafahamu shida za wananchi hawa wanazozipata nikasema nitatoa vitambulisho. Kwa mwenye kitambulisho nilisema afanye biashara kokote na asihonge hata senti tano, akija Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya au Waziri mimi ndiye bosi wao mwenye kitambulisho afanye biashara kokote,” alisema Rais Magufuli na kuongeza;
"Narudia tena kusema kwa viongozi wote ndani ya Serikali, mwenye kitambulisho hatakiwi kuombwa hela yoyote kwa sababu wamelipia mwaka mzima, kuwatoza tena kodi wakati walishalipia kile kitambulisho huo ni wizi.
“Naomba msiwabughudhi wenye vitambulisho, lakini ambao hawana wachape, wale wenye maduka msiwabane katika biashara zao, hawa na wao wanalipia.
“Kwa sababu huyu mwenye duka naye analipa kodi kubwa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania)… na ninyi machinga msiende mkaziba biashara ya mtu, huyu naye analipa kodi kubwa kuliko ninyi.”
Hata hivyo Rais Magufuli amewaomba wananchi mkoani Kagera kuendelea kushirikiana na serikali kulinda amani ya nchi pamoja na kuiunga mkono kwa kufanya kazi ili kufikia azma ya uchumi wa kati na viwanda.