Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapongeza wananchi Chato mkoani Geita kwa kuitikia wito wa Serikali ya Tanzania kuongeza kwenye uzalishaji mali, hatua iliyochangia wilaya hiyo kupiga hatua za maendeleo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Julai Mosi, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Gerson Msigwa imesema Rais Magufuli ametoa pongezi hizo wakati akiwasalimia wananchi hao katika eneo la Njiapanda, muda mfupi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Chato akitokea Dar es Salaam.
Katika taarifa hiyo, imeeleza kuwa akiwa angani Rais Magufuli amefurahishwa kuona namna wananchi wa Chato walivyochangamka kimaendeleo kwa kujenga nyumba za kuishi za kisasa, majengo ya biashara, majengo ya huduma za jamii na mashamba ya mazao mbalimbali.
“Nawapongeza wakazi wa Chato, mnachapa kazi kwelikweli na maendeleo yanaonekana. Chato inabadilika, nilishasema asiyefanya kazi na asile, tuendelee kushikamana,” amesema Rais Magufuli.
Mbali na hilo, Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, kushikamana na kutobaguana ili kulijenga Taifa kwa pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli yupo katika Kijiji cha Mlimani wilayani Chato kwa ajili ya mapumziko.