Na Issa Mtuwa “WM”– Ikulu DSM
Tukio kubwa la kihistoria lililofanyika Ikulu jijini Dar es salaam tarehe 24/07/2019 la kupokea na kukabidhiana dhahabu yenye uzito wa Kg. 35 iliyokamatwa Kenya ikitokea Tanzania ndio lililo wafanya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Madini Doto Biteko kuongelea sekta ya madini kwa lugha ya “kitakwimu” (Namba).
Katika tukio hilo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo iliyokamatwa Kenya baada ya kutoroshwa kutoka Tanzania siku ya tarehe 15/02/2018 baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kukamatwa Kenya. Dhahabu hiyo ililetwa Tanzania na mjumbe maalum ambae pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma alie tumwa na Rais Uhuru Kenyata kuja kukabidhi dhahabu hiyo.
Akizungumzia mafanikio katika sekta ya madini mara baada ya kupokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo, Rais Magufuli alisema, tangu afanye mageuzi makubwa katika sekta ya madini sambamba na marekebisho ya sheria kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Alisema kuanzishwa kwa wizara maalum ya kusimamia madini, ujenzi wa ukuta huko Mirerani, uanzishwaji wa masoko ya madini na marekebisho ya sheria vimekuwa chachu ya mafanikio katika sekta hiyo.
Rais Magufuli aliyataja baadhi tuu ya mafanikio hayo kuwa ni kupunguza kodi nyingi kwa wachimbaji wadogo, pia tangu mwezi Machi 2019 jumla ya masoko 28 ya madini yameanzishwa nchini kote, ongezeko la mapato kutoka sekta ya madini ambapo mwaka 2017/2018 malengo ya makusanyo yalikuwa bilioni 191 lakini wizara ilikusanya bilioni 301 sawa na ongezeko la bilioni 110, mwaka 2018/2019 malengo yalikuwa kukusanya bilioni 310 lakini ikakusanywa bilioni 335 sawa na ongezeko la bilioni 25 na mwaka wa fedha 2019/2020 imekadiriwa kukusanya bilioni 470.35.
Kwa upande wa udhibiti wa matukio ya utoroshwaji wa madini, Rais Magufuli alisema, katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya matukio 102 yaliripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye uzito wa gramu 163, 566,416.45 na Carat 6826.68 huku thamani ya madini yote ikikadiriwa kuwa na zaidi ya bilioni 45.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, alisema takwimu za mauzo kwenye masoko ya madini kumekuwa na mafanikio makubwa. Alisema mpaka sasa zaidi madini yenye thamani ya bilioni 136.7 yameuzwa kwenye masoko yote nchini na serikali imepata mrabaha na clearance fee ya jumla ya bilioni 7.7. Aliongeza kuwa dhahabu iliyokuwa inakusanywa kwa mwaka sasa wanakusanya kwa siku moja kutokana na uwepo wa masoko hayo.
“Mhe. Rais pale Chunya kwa mwaka tulikuwa tunakusanya Kg. 12 lakini tunavyo zungumza tangu kuanzishwa kwa soko lile tarehe 21/03/2019 mpaka leo tarehe 24/07/2019 jumla ya Kg. 270 zimeuzwa kwenye soko hilo”. Alisema Biteko.
Kwa upande wa utoaji wa leseni za uchimbaji, Biteko alisema tangu mwaka 2010 wizara haijawahi kutoa leseni kubwa zenye gharama ya USD 100, lakini mwaka huu wanakwenda kutoa leseni mbili kubwa ambapo mchakato wake umekamilika. Aliongeza kuwa leseni 2673 za wachimbaji wadogo zimetolewa huku leseni za uchimbaji wa kati 32 na leseni 105 za utafiti wa madini zimetolewa. Biteko aliongeza kuwa mwaka huu pia watatoa leseni 2 ya Refinery kwa ajili ya dhahabu na 1 ya Smelter.
Kuhusu wanao hujumu masoko ya madini alisema teyari wamesha ukamata mtandao wa wanaohujumu masoko hayo na mpaka sasa watu 12 wamekamtwa wanaendelea “kupatiwa elimu” polepole na vyombo vya dola.
Akimalizia maelezo yake ya kitakwimu kwa Mhe. Rais, Biteko alimwambia Rais kuwa wizara yake inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi na kwa upande wa Tume ya Madini pekee inahitaji watumishi 220 hivyo anaomba kibali chake waweze kuajiri watumishi hao ili kuongeza ufanisi wa wizara yake.
Social Plugin