Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi amesema hajafurahishwa na kitendo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba kutumia picha waliyopiga pamoja mitandaoni muda mfupi baada uteuzi wake kutenguliwa na Rais Magufuli.
Katika picha hiyo, ambayo January aliiweka muda mchache baada ya rais kutengua uteuzi wake ikimuonyesha yeye na Mwinyi wamekaa kwenye viti viwili tofauti, ambapo aliandika;
“Kwa kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa. Nitasema zaidi siku zijazo.”
Mwinyi amesema hakuona ubaya wa picha ile na wala hakuchukizwa nayo kwa sababu watu wengi wanaokwenda kumuona humuomba picha ya ukumbusho lakini kilichomshangaza ni kitendo cha kutumia picha hiyo katika kipindi hichi.
“Kwa kweli sikupenda kuona picha ya namna ile katika mazingira haya, ile ni picha ya kawaida maana watu wengi wanakuja kuniona na tukishamaliza kuzungumza wanasema tupate ukumbusho na tumefanya sana kwa mtu mmoja mmoja na kwa watu wengi sana kwahiyo nimestaajabu nilipoona imewekwa wakati huu.
“Kijana yule amendika kitabu na aliniomba nimsaidie kuandika dibaji, inawezekana alifanya kama kushukuru lakini silaumu wala sioni vibaya ila kwanini ikawe katika mazingira haya wakati maji yamekorogeka.
”Ile picha ni ya zamani lakini mambo yametokea leo na huko zamani tulikuwa na sababu ya kufanya hivyo kwasababu na mimi nilishika nafasi hii lakini pia kulikuwa na uhusiano wa kitabu chake alichokiandika maana si cha sasa hivi kiliandikwa zamani lakini kwanini ikawa sasa hivi hili kidogo limenishtua,” amesema Mwinyi.
==> Msikilize hapo chini
Social Plugin