RC GAGUTI AAGIZA MAWAKALA WANAOPOTOSHA WAKULIMA WA KAHAWA WAKAMATWE


Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Kagera
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti ameagiza kukamatwa mara moja mawakala wa kampuni binafsi wanaopita vijijini katika wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera na kuwalaghai wakulima wa kahawa wasikubaliane na mfumo wa serikali wa kukusanya Kahawa katika vyama vya msingi na kuziuza kwa mfumo wa ushirika ulioanzishwa na serikali.

Mh.Gaguti ametoa maelekezo hayo Julai 21 2019 katika mkutano wa vyama vya msingi,watendaji wa kata na viongozi wa chama kikuu cha ushirika cha KDCU LIMITED wilayani Karagwe Mara baada ya kukagua viwanda vitatu vya kukoboa Kahawa vya Karim Amri, ASU Company limited na KDCU Limited kuona namna gani vinavyoendelea kuchakata kahawa.

"Nimeona nije kujionea msimu unaendeleaje na kama kuna changamoto yoyote tuitatue kwa pamoja na si kusubiri msimu umeisha.

"Nia ninazo taarifa kuwa kuna mawakala wawili wa kampuni binafsi wamekuwa wakipita vijijini kupotosha wakulima wasifuate mfumo wa serikali ili baadaye wanunue kahawa yao kwa bei ndogo tu, namuagiza kamanda polisi mkoa mawakala hao wakamatwe mara moja", amesema Gaguti.

Amesema maelekezo ya serikali yako wazi kuwa kama kuna mfanyabiashara yeyote anataka kununua Kahawa awasiliane na ofisi yake lakini awe na bei inayomnufaisha mkulima huku akidai kuwa mpaka sasa hakuna mfanyabiashara aliyekidhi vigezo.

Mkuu huyo wa mkoa ameagiza wakuu wa wilaya mkoani hapa kubuni maeneo yenye changamoto ya mtandao kuhakikisha wakulima wanalipwa malipo yao ya awali na wakulima ambao malipo yao yako chini ya laki moja hawatalipwa kwa njia ya mtandao watachukua fedha zao kwa simu za mkononi.

Vyama vikuu vya ushirika mkoani Kagera vya KCU 1990 LTD na KDCU LIMITED tayari vimekusanya Kahawa kilo milioni 8.5 sawa na asilimia 20% ya malengo ya ukusanyaji katika msimu huu wa mwaka 2019/20 na jumla ya shilingi bilioni 6.2 tayari zimelipwa kwa wakulima.

Aidha KDCU LIMITED tayari kimekusanya Kahawa ya maganda kilo 5.8 na shilingi Bilioni 5.3 zimelipwa kwa wakulima sawa na asilimia 15% ya matarajio ya makusanyo.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti akizungumza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم