Wananchi mkoani Kagera wametakiwa kukemea kwa nguvu na kukataa kujihusisha na vitendo vya rushwa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Julai 16,2019 na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera, Mhe. Wilfred Muganyizi Rwakatare (CHADEMA) wakati akizungumza na Malunde1 blog.
Rwakatare amesema wananchi wanapaswa kukataa na kukemea vitendo vya rushwa vinavyoweza kufanywa na kundi la mtu au hususani viongozi wanasiasa ambao ni wagombea badala yake wajikite katika kuangalia mtu atakayewaletea maendeleo katika maeneo yao ili kuweza kufikia azma ya serikali ya viwanda.
"Wananchi mkoani hapa hususani Jimbo la Bukoba mjini wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ili pindi tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa na tume ya uchaguzi nchini waweze kuchagua wanaowataka",amesema.
"Rushwa ni ugonjwa sugu unaokwamisha maendeleo ya nchi na natoa wito kwa wananchi kuwaripoti mara moja kwenye vyombo vinavyohusika wale wrote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi",ameongeza.
Na Lydia Lugakila- Malunde1 blog Bukoba
Social Plugin