Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandishi Isack Kamwelwe amezindua safari ya kwanza ya kimataifa ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ya kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Mumbai India.
Waziri Kamwelwe amezindua safari hiyo, jana, Jumatato, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwenye jengo jipya la safari za kimataifa ‘Terminal 3’ ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Katika hafla hiyo Waziri Kamwelwe amewapongeza Watanzania wote ambao wamekuwa waaminifu kulipa kodi kwa serikali, akisema ndio waliowezesha ununuzi wa ndege 6 za shirika hilo na ujenzi wa jengo hilo jipya.
“Ni jitihada zenu kwenye ulipaji kodi ndizo zimewezesha kufikia mafaniko haya makubwa pamoja na mengine mengi yanayokuja, ni lazima mjipongeze,” ameeleza.
Ameongeza kuwa safari za kimataifa zitasaidia sana katika kukuza biashara na uwekezaji nchini, kuongeza shughuli za utalii, kuunganisha nchi na wananchi wake na mataifa mengine duniani, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Social Plugin