Nigeria na Senegal zimefanikiwa kupenya na kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya kandanda ya mataifa ya Afrika AFCON inayoendelea kutimua vumbi nchini Misri.
Ilianza Senegal kuitupa nje Benin kwa kuichapa 1-0 Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo, bao pekee la kiungo wa Everton, Idrissa Gana Gueye dakika ya 69 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane.
Mane alitumbukiza mipira miwili nyavuni, lakini mara zote mabao yake yalikataliwa kwa Msaada wa Teknolojia ya Video (VAR) na Benin ikamaliza pungufu baada ya Olivier Verdon kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 82
Nigeria iliiadhibu Afrika ya Kusini bao 2 kwa 1 huku goli la ushindi likiwekwa wavuni kutoka mpira wa kona uliochongwa vizuri na William Ekong, dakika moja kabla ya mchezo kumalizika.
Samuel Chukwueze aliipatia Nigeria bao la kuongoza katika dakika 45 za kwanza za pambano lililopigwa katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa mjini Cairo.
Kocha wa Nigeria Gernot Rohr alisema baada ya mchezo kwamba ilikuwa bahati walifanikiwa kupata bao la pili lililofanikisha ushindi na akaongeza kuwa amejawa furaha kutokana na mafanikio ya timu yake kwenye mchezo wa robo fainali.
Katika mchezo huo, Afrika Kusini ilisawazisha mnamo dakika ya 71 kwa goli maridhawa lililowekwa wavuni na mshambuliaji wake Bongani Zungu.
Goli hilo nusura likataliwe baada ya mshika kibendera kusema ulikuwa mpira wa kuvizia lakini hilo lilisawazishwa baadaye na teknolojia ya msaada wa vidio kwa waamuzi wa kandanda, maarufu kama VAR.
Goli la Zungu lilikuwa moja ya magoli matatu yaliyoamuliwa na teknolojia ya VAR katika siku ya kwanza ya kutumiwa teknolojia hiyo kwenye michuano ya AFCON.
Maamuzi yote matatu kuhusu magoli wakati wa mechi mbili za jana yalitoa ushindi.
Teknolojia ya msaada wa vidio kwa waamuzi wa kandanda, VAR, itaendelea kutumika katika michezo itakayopigwa leo na hadi mchezo wa mwisho wa fainali za AFCON.
Social Plugin