NAIBU Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema Serikali kupitia Tume ya Tafa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) imetoa kiasi cha Tsh Milioni 700 kwa wabunifu 60 ili kuendeleza tafiti na bunifu zao na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.
Akizungumza leo Jumatano (Julai 10, 2019) wakati wa Kongamano maalum la Ubunifu lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na COSTECH katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), Ole Nasha alisema Serikali itaendelea kuwatambua wabunifu na wagunduzi wa kazi mbalimbali nchini.
Ole Nasha alisema kwa sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na bunifu za kazi mbalimbali lakini zimeshindwa kutambulika na hivyo kuilazimu Serikali kuanza kuweka utaratibu maalum ikiwemo kuandaa mwongozo unaotarajiwa kuwatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali.
“Mwaka jana tuliandaa mashindano maalum ya ubunifu na walipatikana washindi wa kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalum wenye utaratibu wa kuendesha vituo vya teknolojia na ubunifu” alisema Ole Nasha.
Aidha Ole Nasha aliitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuandaa kongamano la kila mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wabunifu hao kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini kazi mbalimbali za wabunifu na watafiti na kuweza kutambulika.
Kwa mujibu wa Ole Nasha alisema wabunifu na wagunduzi nchini kutambua kuwa masuala ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na kuwataka wabunifu wasio katika sekta rasmi kuendelea kubuni bidhaa na vifaa mbalimbali kwa kuwa COSTECH si taasisi inayowagusa wasomi peke yao bali wabunifu wote waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifafanua zaidi Ole Nasha alisema kutokana na wabunifu na watafiti wengi kukabiliwa na changamoto ya kuibiwa kazi zao, aliitaka COSTECH kukaa pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA) ili kuhakikisha kuwa wabunifu wanawekewa utaratibu maalum kwa ajili ya kulinda bunifu zao.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Prof. James Mdoe alisema Serikali itaendelea kuzitambua kazi mbalimbali za wabunifu na wagunduzi nchini ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano madhubuti kwa ajili ya kutambua na kuendeleza kazi za ubunifu na ugunduzi nchini.
Naye Mbunifu wa Maji taka kutoka Kampuni ya Biocon Africa Ltd, Prof. Karoli Njau aliitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wabunifu na wagunduzi wote nchini ili waweze kuonyesha kazi zao na kuhakikisha kuwa kuna utaratibu mzuri wa kuwapata watoa huduma katika kazi mbalimbali zinazoweza kupatikana nchini.
Social Plugin